1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waidhinisha ushuru mkubwa kwa gari za China

4 Oktoba 2024

Umoja wa Ulaya umeidhinisha nyongeza kubwa ya ushuru wa forodha kwa magari ya umeme yanayoundwa nchini China, licha ya upinzani mkali kutoka Ujerumani na wasiwasi kwamba uamuzi huo utazusha vita vya kibiashara na China.

China | Leapmotor E-Auto
Gari za umeme kutoka China.Picha: Caroline Chen/AP Photo/picture alliance

Duru kutoka mjini Brussels zinasema mataifa 10 wanachama, yakiwemo Ufaransa, Italia na Poland, yameridhia kutozwa nyongeza ya hadi asilimia 35.5 ya ushuru kutoka viwango vya sasa vya asilimia 10 kwa magari yote ya umeme yanayoingizwa kutoka China.

Nchi tano za Umoja huo, zikiwemo Ujerumani na Hungary, zimepinga hatua hiyo zikitoa hadhari kwamba itachochea vita vya kibiashara na China, ambayo ni moja ya washirika muhimu wa kibiashara wa kanda hiyo. 

Soma zaidi: Orban atahadharisha Ulaya, China zaelekea vita vya kiuchumi

Umoja wa Ulaya unaituhumu China kutoa ruzuku ya kuyasaidia makampuni yake ya kuunda magari, mwenendo ambao unapunguza ushindani na kuvidhoofisha viwanda vya mataifa ya Ulaya.