1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waijadili Uturuki

14 Novemba 2016

Mawaziri wa masuala ya nje wa Umoja wa Ulaya leo hii wametafuta namna ya kuwa na msimamo wa pamoja, wakati ambapo wanajadili mahusiano ya umoja huo na Uturuki.

Türkei Präsident Recep Tayyip Erdogan
Picha: Picture-Alliance/dpa/S. Sunat

Hata hivyo baadhi ya mawaziri hao wanataka kuwepo kwa uvumilivu na wengine wakitaka kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya serikali na namna inavyoshughulika na mkwamo kwenye masuala yahusuyo vyombo vya habari na upinzani nchini humo. 

Hatua zinazochukuliwa na rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan baada ya mapinduzi yaliyofeli, mnamo mwezi Julai zimeibua wasiwasi juu ya mahusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, kufuatia kufungwa kwa wanachama kutoka vyama vya siasa vya upinzani, pamoja na kile kinachoelezwa kuwa ni kulisafisha jeshi na mashirika ya umma kumetajwa kuongeza ukosoaji kutoka kona mbalimbali.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukifanya jitihada za kuzungumza na Uturuki, ambayo tangu mwaka 1999 imekuwa ikiwania uanachama ndani ya jumuiya hiyo. Hata hivyo mchakato wa kuipatia nafasi hiyo umekuwa ukisuasua. Hatua za hivi karibuni ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Uturuki zimetoa msukumo mpya kwa baadhi ya wanachama wa bunge la Umoja huo wa kutaka kuahirishwa kwa mazungumzo na nchi hiyo ya kuomba uanachama wa umoja wa Ulaya.

Linapokuja suala la haki za bianadamu, Uturuki na utawala wa sheria, Uturuki imeendelea kujisogeza mbali zaidi na Ulaya, amesema waziri wa mambo ya nje wa Austria Sebastian Kurz, kabla ya kuanza kwa mkutano huo leo hii mjini Brussels. "Uturuki haina nafasi ndani ya Umoja wa Ulaya", ameongeza Kurz.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema mazungumzo dhidi ya Uturuki yanaendelea, ingawa tayari wamekwishatoa mtizamo wao juu ya hali ya mambo ambayo tayari yamejitokeza nchini humo. Mawaziri hao watapata nafasi ya kubadilisha mawazo juu ya namna hali ya mambo ilivyo nchini humo.

Waandamanaji wakiwa mitaani kupinga baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Rais Erdogan nchini Uturuki.Picha: picture-alliance/AP Photo/Francois Mori

Ulaya imekwishaionya Uturuki kwa hatua zake.

Wiki iliyopita, Umoja wa Ulaya ulitoa onyo kali dhidi ya Uturuki kuhusiana na hatua zake zinazokwenda kinyume na masuala muhimu ya utawala wa sheria na uvunjwaji wa haki za binadaamu, huku watendaji wa juu ya Umoja huo wakihoji kuhusu mazunguzmo kuhusu nia ya Uturuki ya kuomba uanachama kwenye Umoja wa Ulaya. 

Mahusiano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya yalitiwa msukumo zaidi kupitia makubaliano kuhusiana na masuala ya uhamiaji, ambapo Uturuki inasaidia kupunguza idadi ya wahamiaji wanaoingia Barani Ulaya. Hata hivyo Uturuki, mara kwa mara imetishia kujiondoa kwenye makubaliano hayo kutokana na kuzuiwa kwa raia wake kusafiri bila visa ndani ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Wanachama wa umoja huo wanachukulia hatua hiyo kama kitisho kinachpoweza kuruhusu wahamiaji wengi zaidi kuingia Ulaya, baada ya wengine Milioni moja, pamoja na waomba hifadhi kuingia barani humo mwaka uliopita.

Katika hatua nyingine, mawaziri hao wa mambo ya nje wamethibitisha tena mpango wao wa kuiunga mkono Iran kwenye makubaliano juu ya nyuklia, ambayo rais mteule wa Marekani Donald Trump ameyeita kuwa ni makubaliano mabaya zaidi kufikiwa duniani, na kuapa kutoyaunga mkono.

Mawaziri hao wamesema Umoja wa Ulaya utaendelea kusisitiza bila ya kubadilika kuhusiana na msimamo wake huo ambao unaungwa mkono na mataifa yenye nchuvu ndani ya Umoja huo ambayo ni pamoja na Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, pamoja na China, Marekani na Urusi. 

Trump, kwenye kampeni zake aliuita mkataba huo kama "Janga, na makubaliano mabaya ambayo hayajawahi kufikiwa duniani" na kueleza wazi kuiondoa Marekani kwenye makubaliano iwapo atakuwa rais, ingawa amekiri itakuwa vigumu kujiondoa kwenye mkataba huo uliopo kwenye makubaliano ya Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Saumu Yusuf