1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ursula von der Leyen anazitembelea nchi za Amerika Kusini

12 Juni 2023

Umoja wa Ulaya hivi sasa unaiona haja ya kuijongelea kanda ya Amerika Kusini kutafuta mbadala wa China.

Tschechien Prag | Pressekonferenz Ursula von der Leyen
Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.Picha: Lukas Kabon/AA/picture alliance

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameanza ziara yake ya kuyatembelea mataifa manne ya Amerika ya Kusini, ikiwa na lengo la kuimarisha mahusiano ya kisiasa na kibiashara ya umoja huo.

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen katika ziara yake hii atakutana na marais wa Brazil, Argentina, Chile na Mexico wakati atakapofika kwenye mataifa yao.

Soma pia: Von der Leyen awarai viongozi wa Ulaya kushikamana kuikabili China 

Ni ziara ambayo lengo lake ni kuimarisha mahusiano ya kisiasa na kibiashara ambayo Umoja wa Ulaya unakiri kwamba umekuwa baadhi ya wakati ukiupuuza.

Ziara ya Ursula Von Der Leyen imekuja pia katika wakati ambapo Umoja huo wa Ulaya mjini Brussels unajiandaa pia kuwakaribisha zaidi ya viongozi 30 kutoka kanda hiyo ya Amerika ya Kusini na Caribean katika mkutano wa kilele tarehe 17 hadi 18,ukiwa ni mkutano wa kile kinachoitwa  ajenda mpya  katika ukanda huo iliyozinduliwa wiki iliyopita.

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine,Umoja huo wa Ulaya umekuwa ukitafuta washirika wenye mtazamo sawa na wake ili kupata vyanzo vingine vya kibiashara pamoja na madini muhimu inayoyahitaji kwaajili ya kuingia kwenye enzi mpya ya kijani na kulisaidia bara hilo kupunguza utegemezi wake kwa China.

Borrell: Uhusiano kati ya EU na Amerika Kusini unahitaji kuimarishwa 

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: Frederick Florin/AFP via Getty Images

Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Josep Borrell hivi karibuni alisema kwamba ushirikiano na kanda hiyo umekuwa baadhi ya wakati haupewi umuhimu au hata kupuuzwa na unahitaji hivi sasa kuimarishwa pamoja na wale aliowaita  washirika watakaopendelewa na Umoja huo.

Ziara yake hiyo inafuatia ile ya Kansela wa Ujerumano Olaf Scholz aliyoifanya mwanzoni mwa mwaka huu na pia imekuja wiki moja kabla ya rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva kuelekea Paris nchini Ufaransa.

Soma pia: Von der Leyen afanya ziara nchini Marekani 

Katika ziara ya Von der Leyen yaliyotanguliwa kwenye ajenda ya mazungumzo ni suala la makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa mwaka 2019 baina ya Umoja huo na kundi la nchi nne ambazo ni Argentina, Brazil, Paraguay na Uruguay lakini makubaliano hayo yalisimamishwa,kwa kiasi kikubwa kutokana na wasiwasi kuhusu uharibifu wa msitu wa Amazon.

Umoja wa Ulaya unatarajia kupata jibu la kundi hilo haraka kuhusiana na pendekezo lake lililosisitiza kuhusu suala la kuwepo uendelezwaji wa makubaliano hayo pamoja na ahadi za kushughulikiwa suala la mabadiliko ya tabia nchi katika mkataba huo.

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva akifanya mazungumzo na rais wa zamani wa Colombia Ernesto Samper.Picha: Bruna Prado/AP/picture alliance

Kadhalika rais huyo wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya atataka kulitilia msukumo suala la makubaliano ya kibiashara kati ya Umoja huo na Mexico uliofikiwa na pande hizo mbili mnamo mwaka 2018.

Lakini pia suala jingine litakalopewa kipaumbele kwenye ziara hiyo ni nia ya Umoja wa Ulaya ya kutaka ushirikiano na nchi kadhaa za kanda hiyo kuhusu bidhaa ghafi muhimu inazohitaji.

Tayari umeingia makubaliano na nchi kama Chile ambayo inaweza kuyapatia makampuni ya Umoja wa Ulaya fursa ya kuchimba Lithium na shaba.

Kuna uwezekano pia wa kufikia maelewano na Argentina ambayo huenda pia ikatoa nafasi ya wawekezaji wa Umoja wa Ulaya kuchimba mafuta na gesi asilia katika hifadhi yake ya Vaca Muerta.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW