1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waitaka Ethiopia irudishe mawasiliano Tigray

4 Desemba 2020

Wanajeshi wa Ethiopia pia watuhumiwa kuwazuia wakimbizi wanaokimbia vita Tigray kukimbilia Sudan na mpaka wake wa kuingia upande wa Hamdayet Sudan umefungwa.Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wataka vita visitishwe

Äthiopier Flüchten vor Kämpfen in Tigray in den Sudan
Picha: Mohamed Nureldin Abdallah/REUTERS

Kamishna wa Umoja wa Ulaya kuhusu usimamizi wa migogoro ameitolea mwito serikali ya Ethiopia kurudisha mawasiliano katika jimbo la Tigray. Lakini pia amezitaka pande zote zinazopambana katika jimbo hilo kusitisha vita.

Janez Lenarcic ni Kamishna wa Umoja wa Ulaya kuhusu usimamizi wa migogoro na yuko nchini Sudan ambako amekwenda kutazama hali ya wakimbizi wakiiethiopia waliokimbia vita Tigray ilivyo nchini humo.Jana Alhamisi akizungumza kutoka kambi ya Um Raquba ambako alikutana na wakimbizi hao na kuzungumza nao alisema wito mkubwa anaoutowa kwa serikali ya mjini Addis Ababa ni kufungua njia za mawasiliano iliyoyafunga katika jimbo la Tigray. Kamishna huyo wa Umoja wa Ulaya ameeleza kwamba amezungumza na wakimbizi kadhaa kwenye kambi hiyo na kile kilichomsikitisha zaidi ni kusikia kwamba wakimbizi hao hawana taarifa yoyote kuhusu jamaa zao wala marafiki zao waliowaacha Tigray.

Picha: Nariman El-Mofty/AP/picture alliance

''Unajua hata bado hatujafika,misafara iliyokuwa ikipeleka msaada kwenye eneo hilo kabla ya vita kuanza ilisimama baada ya operesheni ya kijeshi na mpaka sasa bado  haijaweza kuondoka,,hiyo ndiyo hali iliyopo. Kuhusu msaada mpya wa kibinadamu ambao utayaangalia mahitaji mapya yaliyojitokeza kutokana na vita hivi, ni lazima kwanza tutathmini kinachohitajika. Acha niseme tu kwamba moja ya sababu kwa nini nimekuja hapa ni kwamba wakimbizi wakitigrai wako hapa na siwezi kuingia Tigray kwahivyo nimekuja hapa''

Kimsingi Jumatano Ethiopia ilitangaza rasmi kwamba inaruhusu Umoja wa Mataifa kupeleka msaada Tigray kwa mujibu wa makubaliano yaliyoonekana na shirika la habari la AFP.

Na kwenye makubaliano hayo imeelezwa wazi kwamba Umoja wa Mataifa na washirika wake katika masuala ya kiutu wanaweza kuwapelekea msaada raia kwenye maeneo yanayodhibitiwa na serikali ndani ya jimbo hilo la Tigray. Ingawa leo Ijumaa Umoja huo wa Mataifa umelalamika kwamba vita vinaendelea na juhudi za kupeleka msaada zinatatizwa.

Lakini pia upande mwingine taarifa zilizotoka kwa wanajeshi wa Sudan waliokataa kutajwa majina zinasema wanajeshi wa serikali kuu ya Ethiopia jana waliwazuia watu waliokuwa wakilikimbia jimbo la Tigray kuvuka mpaka kuingia upande wa mpaka wa Hamdayet, Sudan. Matukio hayo yanafuatia madai mengine kama hayo yaliyotolewa na wakimbizi siku kadhaa za nyuma wakieleza kwamba wanajeshi wa Ethiopia waliwasimamisha na kuwazuia kuondoka Tigray.

Picha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Wanajeshi wa Sudan wanasema waliweka usalama kwenye eneo hilo na baadaye jana jioni mpaka huo ulifungwa na pia waandishi habari wa shirika la habari la Associated Press wanasema waliona watu kadhaa wakiwa wanasubiri katika eneo hilo la mpaka upande wa Ethiopia.Mkuu wa masuala ya wakimbizi katika Umoja wa Mataifa Filipo Grandi alipoulizwa ikiwa taarifa hizo anazijua alisema timu yake bado haijazungumza suala hilo la serikali ya Ethiopia.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo