1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waitaka Uturuki kuhifadhi wahamiaji

15 Oktoba 2015

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya leo watakutana katika mkutano wa kilele, kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa wahamiaji barani Ulaya pamoja na kuishawishi Uturuki kuwapa hifadhi wahamiaji wanaotokea Syria

Brüssel Jean-Claude Juncker Treffen mit türkischem Präsidenten Tayyip Erdogan
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker akiwa na Rais wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: Reuters/F. Lenoir

Mkutano huo wa kilele unalenga kufanya kazi pamoja na nchi zilizo nje ya mipaka ya bara la Ulaya ili bara hilo liweze kupambana na mgogoro mkubwa wa wahamiaji kuwahi kutokea tangu vita vya pili vya dunia.

Jambo muhimu litakalozingatiwa katika mkutano huo wa leo ni kuishawishi Uturuki kuukubali mpango wa Umoja wa ulaya, unaoitaka nchi hiyo kuwapa hifadhi wahamiaji milioni mbili, huku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa anelekea nchini humo Jumapili kwa ajili ya mazungumzo.

Merekel asisitiza mshikamano barani Ulaya

Kabla ya mkutano huo wa kilele, Merkel amesema Uturuki ina jukumu muhimu katika kuutatua mgogoro wa wahamiaji, na kwamba nchi za Ulaya zinahitajika kuisaidia zaidi nchi hiyo kupambana na ongezeko hilo la wahamiaji.

Merkel ameongeza kwamba lazima kuwepo mshikamano barani Ulaya juu ya mgogoro wa wahamiaji

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa katika bunge la Ujerumani - BundestagPicha: Reuters/H. Hanschke

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Umoja wa Ulaya Frans Timmermans pamoja na maafisa waandamizi wingineo, wamewasili Uturuki jana kuishinikiza serikali ya nchi hiyo kukubali mpango huo wa Umoja wa Ulaya, baada ya kuahirisha safari hiyo kutokana na shambulio la mabomu la mjini Ankara mwishoni mwa juma lilopita.

Akiwa anaelekea katika mkutano huo wa kilele, Rais wa baraza la kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, amesema makubalino pamoja na Uturuki yatakuwa na tija iwapo yatasaidia kupunguza mmiminiko wa wahamiaji barani Ulaya.

Viongozi wa Ulaya wanatarajia kwamba kuwasaidia wahamiaji wa Syria waliopo Uturuki, kwa kuwapa fedha pamoja na kukiimarisha kikosi cha walinzi wa pwani cha nchi hiyo, kutawakatisha tamaa kufanya safari hatari ili kuingia barani Ulaya.

Uturuki yakataa kambi zaidi za wahamiaji

Akiwa mjini Brussels wiki iliyopita, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, amesema nchi yake inahitaji fedha zaidi na inakataa pendekezo la kuongezwa kwa kambi za wahamiaji.

Erdogan pia amesema Uturuki inahitaji ushirikiano zaidi kutoka Umoja wa Ulaya katika kampeni yake ya kupambana na ugaidi dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi pamoja na kundi la Dola la Kiislamu IS.

Bila ya kuwepo kwa dalili yoyote inayoashiria kumalizika kwa vita vilivyodumu zaidi ya miaka minne sasa nchini Syria, katika miezi ya hivi karibuni Umoja wa Ulaya umekuwa ukisistiza msimamo wake juu ya mmiminiko wa wahamiaji ambao wameshatimia karibu 600,000 barani humo kwa mwaka huu pekee.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe

Mhariri: Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW