Umoja wa Ulaya waiwekea vikwazo Mali
23 Machi 2012Uamuzi huo umefikiwa mjini Brussels kufuatia kikao kilichofanywa na mawaziri hao siku ya Ijumaa Machi 23 mwaka huu. Kwenye tamko lao la pamoja mawaziri hao wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya walilaani vikali kitendo kilichofanyywa na wanajeshi wa Mali na kuwataka kusitisha mapigano mara moja.
Tamko hilo pia limejumuisha amri ya kuwataka wanajeshi hao kuwaachia huru maafisa wa serikali wanaowashikilia akiwemo aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Amadou Touman Toure.
Kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa nchini Mali, nimeamua kusitisha kwa muda shughuli zote za maendeleo zinazofanywa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya nchini humo hadi hapo hali itakaporejea na kuwa kama inavyotakiwa." alisema Kamishna wa Masuala ya Maendeleo wa umoja huo Andris Piebalgs.
Akizungumzia mapinduzi hayo Mkuu wa sera za mambo ya nje wa umoja huo Catherine Ashton amesema Umoja wa Ulaya unatumaini kuwa katiba itarejeshwa haraka sana na kwamba nchi itarejea katika utawala wa sheria na matakwa yake.
Nazo Benki ya Dunia pamoja na Benki ya Maendeleo Afrika pia zimeungana na Umoja wa Ulaya kwa kusitisha misaada ya maendeleo nchini Mali.
Wakati vikwazo vya kiuchumi vikianza kuiandama Mali, huko Bamako mji mkuu wa nchi hiyo Kiongozi wa mapinduzi hayo kijeshi Kapteni Amadou Sanogo ametangaza mpango wa kuwapeleka mahakamani Rais wa nchi hiyo na viongozi wake wa juu ambao wanawashikilia hadi sasa.
Pamoja na nia hiyo ya kuwafikisha katika mikono ya sheria viongozi hao, Kapteni Sanogo pia amezungumzia kuhusu usalama wa watu hao na kusema kuwa wako hai chini ya uangalizi mzuri.
"Hawa watu wako salama salimini. Hatutawagusa hata nywele vichwani mwao. Nitawafikisha mahakani ili watu wa Mali wapate kuufahamu ukweli." Alisema Kapteni Amadou Sanogo katika mahojiano na Shirika la Habari la Ufaransa AFP katika kambi ya kijeshi karibu na mji mkuu wa nchi hiyo.
Hata hivyo umoja huo umesisitiza kuwa bado utaendelea kuwasaidia raia wa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa misaada ya moja kwa moja ya kibinaadamu. Mali inakabiliwa na tishio la baa la njaa kufuatia kukumbwa na ukame.
Baraza la Umoja wa Ulaya lilipanga kutumia kiasi cha Euro milioni milioni 583 kwa ajili ya shughuli za maendeleo nchini Mali katika kipindi cha mwaka 2008 na 2013.
Mwandishi: Stumai George /AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman