1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakataa madai ya ACP

25 Septemba 2005

Kisumu, Kenya:

Umoja wa Ulaya umekataa miito ya nchi zinazozalisha sukari za Afrika, Karibiki na Pasifiki, kikundi kinachojulikana kama ACP, ya kuchelewesha utekelezaji wa mapendekezo ya mageuzi ya biashara ya sukari. Nchi za ACP zinadai kuwa mageuzi hayo yataathiri sana uchumi wao unaoendelea vizuri. Mkurugenzi wa Uchumi na Masoko wa Umoja wa Ulaya, Russel Milton, anayehudhuria mkutano huo wa nchi 18 wanachama wa ACP, amesema mjini Kisumu kuwa badala ya nchi hizo kupambana na mabadiliko hayo zinapaswa kuafiki mpango wa Brussels wa kutaka kuwapa ruzuku Wakulima wa sukari watakaoathirika na mageuzi hayo. Bw. Milton ameongeza kusema kuwa nchi za ACP zinapaswa haraka kutayarisha mipango itakayokwenda sambamba na mageuzi hayo ili nchi zao ziweze kunufaika.

Mawaziri wa ACP, wanaokutana Kisumu, Kenya, wanaamini kuwa lengo la Umoja wa Ulaya la kutaka kupunguza bei ya sukari kwa asili mia 39 baada ya miaka miwili kuanzia mwaka 2007 litasambaratisha uchumi wa nchi zao. Makamu wa Rais wa Kenya, Moody Awori, amesema kuwa wako tayari kuongoza mapambano dhidi ya mageuzi hayo ya Umoja wa Ulaya.