1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGabon

EU haina mipango ya kuwaondoa raia wake kutoka Gabon.

31 Agosti 2023

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema kwa sasa umoja huo hauna mipango ya kuwahamisha raia wake kutoka Gabon kwa sababu licha ya mapinduzi hali ni tulivu nchini humo.

Belgien EU-CELAC Josep Borrell im Gebäude des Europäischen Rates in Brüssel
Picha: Francois Walschaerts/AP Photo/picture alliance

 

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amewaambia waandishi wa habari kwamba hali nchini Gabon ni shwari baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyosabisha kuondolewa madarakani Rais aliyechaguliwa tena, Ali Bongo.

Borrell, amesema kwa sasa Umoja wa Ulaya hauna mpango wa kuwahamisha watu wake kutoka nchini Gabon, kwa sababu hali ni shwari na wala hakuna dalili na kutokea vurugu. Wapo takriban raia 10,000 wa Umoja wa Ulaya nchini Gabon lakini mpaka sasa hakuna nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Ulaya iliyoonyesha wasiwasi juu ya hali ya raia wake. 

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell.Picha: Sierakowski/EUC/ROPI/picture alliance

Borrell amebainisha kwamba mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon hayawezi kulinganishwa na mgogoro wa Niger, amesema maafisa wa kijeshi wa Gabon waliingilia kati baada ya rais aliyepinduliwa Ali Bongo kushinda uchaguzi uliokuwa si wa haki.

Soma:Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Afrika walaani mapinduzi ya kijeshi Gabon

Raia wa Gabon na waangalizi wa uchaguzi wamesema uchaguzi huo ulikumbwa na makosa na pia haukufanyika kwa uwazi.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, amesema kwa kawaida, mapinduzi ya kijeshi sio suluhisho, lakini haipaswi kusahaulika kwamba nchini Gabon uchaguzi uliomalizika ulijaa dosari na amehoji kuwa wizi wa kura unaweza kusababisha mapinduzi ya kiraia katika taasisi.

Raia wa Gabon wakisherehekea baada ya jeshi kutangaza kuwa wamempindua rais Ali Bongo.Picha: Gaetan M-Antchouwet via REUTERS

Borrell ameyazungumza hayo kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanaotarajiwa kujadili jinsi ya kuisaidia jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS kushughulikia mapinduzi ya kijeshi ya Julai 26 nchini Niger.

Soma:Jeshi lamtangaza mkuu wa kitengo cha walinzi wa rais Brice Nguema kama kiongozi wa mpito Gabon

Raia wa Gabon wameamka leo hii Alhamisi kwa kuwa na kiongozi mpya wa kijeshi baada ya wanajeshi walioasi kumuondoa rais Ali Bongo, ambaye familia yake ilitawala taifa hilo lenye utajiri wa mafuta kwa zaidi ya miongo mitano. Familia ya Bongo imeshutumiwa kwa ufisadi uliokithiri na kuwanyima idadi ya watu wapatao milioni 2, utajiri wa mafuta wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Rais wa Gabon aliyepinduliwa Ali Bongo Ondimba.Picha: TP advisers on behalf of the President's Office/AP Photo/picture alliance

Kiongozi mpya ni Jenerali Brice Clotaire Oligui Nguema, mkuu wa kitengo maalum cha walinzi. Jeshi lilimtangaza Nguema kwenye Televisheni ya serikali saa chache baada ya Rais Ali Bongo Ondimba alipotangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Vyanzo:AFP/AP