1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya washindwa kumshawishi Orban kuhusu Ukraine

20 Machi 2026

Viongozi wa Umoja wa Ulaya Ijumaa wameshindwa kumshawishi Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban kuondoa kizuizi chake katika mkopo wa yuro bilioni 90 wa kuisaidia Ukraine kupambana na uvamizi wa Urusi.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels
Viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini BrusselsPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Baada ya mkutano wa kilele uliofanyika huko Brussels,viongozi kadhaa wameelezea kusikitishwa kwao na Orban.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amemtuhumu Orban,ambaye ana mahusiano mazuri na Rais wa Urusi Vladimir Putin, kwa kufanya kitendo cha "usaliti mkubwa" ambacho kimiharibu sifa ya Umoja wa Ulaya na uwezo wake wa kuchukua hatua.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanasema katika kipindi cha wiki chache zijazo, huenda Ukraine ikaishiwa na fedha iwapo haitopokea mkopo huo.

Orban anazuia kuidhinishwa kwa mkopo huo kutokana na mzozo ulioko katika bomba la mafuta la Druzhba ambalo linabeba mafuta ya Urusi kupitia Ukraine kuelekea Hungary na Slovakia.

Kulingana na Ukraine na Umoja wa Ulaya, bomba hilo liliharibiwa na shambulizi la Urusi mwezi Januari.

Baadhi ya viongozi wa Ulaya wana matumaini kuwa Orban ataubadili msimamo wake bomba hilo litakapokarabatiwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW