1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Umoja wa Ulaya washindwa kupata makubaliano kuisidia Ukraine

15 Desemba 2023

Umoja wa Ulaya umeshindwa kukubaliana juu ya msaada wa euro bilioni 50 kwa ajili ya Ukraine, licha ya kuamua hapo jana kuanzisha mazungumzo ya kujiunga kwa taifa hilo linalokabiliwa na vita.

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa Ulaya wakiwa kwenye mkutano mjini Brussels. Katikati ni waziri mkuu wa Hungray, Victor Orban.Picha: Omar Havana/AP/picture alliance

Msaada huo ulizuwiwa na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, katika pigo jengine kwa Rais Volodymyr Zelenskiy, baada ya hapo awali rais huyo wa Ukraine kushindwa kuwashawishi wabunge wa Marekani kuidhinisha kiasi cha dola bilioni 61, katika fedha za ziada Ukraine, kwa ajili ya kununu silaha kutoka Marekani.

Kuanza kwa mazungumzo ya Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya ulikuwa wakati muhimu na mabadiliko ya kustaajabisha ya msimamo kuelekea taifa lililoko vitani, ambalo lilipambana kutafuta uungwaji mkono wa azma yake ya kuwa mwanachama, na ambalo kwa muda mrefu lilikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa Orban.

Kiongozi huyo wa Hungary alimua kutozuwia mazungumzo ya uanachama, lakini baadae alizuwia utoaji wa fedha za msaada kwa Ukraine.

Maamuzi hayo yalihitaji kuamuliwa kwa sauti moja na viongozi wa mataifa wanachama.

Michel: Mazungumzo ya kuikaribisha Ukraine ni ishara ya matumaini 

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel.Picha: Virginia Mayo/AP/picture alliance

Na licha ya mkwamo juu ya fedha za msaada, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, aliyeongoza mkutano huo wa kilele mjini Brussels ambako uamuzi ulifanyika, alitaja kuanza kwa mazungumzo ya kujiunga kuwa ishara ya wazi ya matumaini kwa watu wa Ukraine na bara la Ulaya.

"Usiku wa leo tulituma ishara nzito kwa raia wa Ulaya, ishara nzito kwa raia wa Ukraine, kwa sababu tumeamua kutoa hadhi ya mgombea kwa Georgia, kufungua mazungumzo na Ukraine na Moldova, kuchukuwa hatua muhimu kwa Bosnia Herzegovina. Huu ni wakati wa kihistoria, Baraza la kihistoria la Ulaya." amesema Michel.

Ingawa mchakato kati ya kufungua majadiliano na hatimaye Ukraine kuwa mwanachama yanaweza kuchukuwa miaka mingi, Zelenskiy alikaribisha makubaliano hayo aliyoyataja kama ushindi kwa Ukraine na Ulaya.

Ukraine inategemea pakubwa fedha hizo kusaidia uchumi wake ulioharibiwa vibaya na vita vya Urusi ili kupita katika mwaka unaokuja.

Mkutano wa kujadili msaada kwa Ukraine kufanyika Januari 

Waziri Mkuu wa Hungary, Victor Orban Picha: Nicolas Economou/NurPhoto/IMAGO

Michel alisema viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya watakutana tena Januari na kujaribu kuondoa mkwamo. Orban alikuwa ameonya kabla ya mkutano huo wa kilele kwamba kulazimisha uamuzi juu ya suala hilo kungeharibu umoja ndani ya EU.

Akizungumza mapema leo katika mahojiano na kituo cha redio ya taifa cha Hungary, Orbanametaka kuachia fedha zote za ufadhili wa Hungary zilizozuwiwa na Umoja wa Ulaya, kabla ya kuzingatia kuondoa turufu yake juu ya msaada wa Ukraine.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo, aliitaja hatua ya kuanzisha mazungumzo ya uanachama na Ukraine kuwa pigo kwa Rais wa Urusi Vladmir Putin, na kuongeza kuwa imetuma ujumbe kwa kiongozi huyo wa Urusi kwamba Ulaya haiko tayari kuiacha Ukraine mikononi mwa Moscow.

Nchini Marekani, mshauri mkuu wa usalama wa taifa Jake Sullivan, alisifu uamuzi wa Umoja wa Ulaya alioutaja kuwa wa kihistoria kuhusu Ukraine na Moldova, akisema ni hatua muhimu katika kutimiza matarajio yao ya Ulaya na Amerika Kaskazini.