Umoja wa Ulaya wataka kupiga marufuku mafuta ya Urusi
4 Mei 2022Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Urusula von der Leyen amependekeza vikwazo vya mafuta kwa awamu dhidi ya Urusi kuhusiana an vita vyake nchini Ukraine, pamoja na kuiwekea vikwazo benki kubwa ya Urusi katika hatua ya kuitenga nchi hiyo.
Iwapo mpango huo utaridhiwa na serikali za nchi wanachama wa umoja huo utakuwa changamoto kubwa kwa ukanda huo wa kibiashara unaotegemea nishati kutoka kwa Urusi na lazima utafute vyanzo mbadala. Rais wa halmashuri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema mpango huo unalenga kufuta uagizaji mafuta ghafi kutoka Urusi katika kipindi cha miezi sita na bidhaa za mafuta yaliyosafishwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
"Leo tunawasilisha awamu ya sita ya vikwazo. Kwanza tunawaorodhesha maafisa wa vyeo vya juu na watu waliofanya uhalifu wa kivita Bucha na wale wenye dhamana kwa kuzingirwa kwa mji wa Mariupol. Hii inatuma ishara nyingine muhimu kwa maafisa wote wa utawala wa Kremlin: Tunawafahamu, tutawabebesha dhamana, hatutawaacha mkimbie kwa makosa haya.
Von der Leyen pia amesema benki ya Sverbank, ambayo ni mojawapo ya benki kubwa za Urusi imefutwa kutoka mfumo wa kufanyia miamala ya fedha wa SWIFT. Benki hii inajumuisha asilimia takriban 37 ya sekta nzima ya benki ya Urusi na pia watazifungia benki nyingine kubwa zisiutumie tena mfumo huo wa SWIFT. Kwa njia hii wataziathiri benki ambazo ni muhimu kwa mfumo mzima wa fedha wa Urusina uwezo wa rais Vladimir Putin kufanya uhabifu.
Televisheni za Urusi zapigwa marufuku Ulaya
Umoja wa Ulaya pia umezipiga marufuku televisheni tatu kubwa zinazomilikiwa na Urusi zisipeperushe matangazo yake Ulaya. Von der Leyen amesema vyombo hivyo vya habari havitaruhusiwa kusambaza maudhui zao tena katika nchi za Umoja wa Ulaya, katika mfumo wowote ule, iwe ni kwa njia ya satelaiti, intaneti au appu za simu za kisasa za smartphone. Amesema wamezitambua televisheni hizo kama vyombo vinavyotumiwa kueneza na kukuza uongo na propaganda ya rais Putin kwa nguvu kubwa na hawapaswi kuzipa uwanja wa kusambaza uongo huo.
Hivi leo vikosi vya Urusi vimefanya mashambulizi ya maroketi katika miji ya mashariki mwa Ukraine na kuua na kuwajeruhi raia kadhaa. Wanajeshi wamekivamia kiwanda cha kutengeneza chuma cha pua mjini Mariupol ambako watu kadhaa walikuwa wakiondoka baada ya kuvumilia wiki kadhaa za mashambulizi ya makombora dhidi ya mji huo, ambao ni ngome ya mwisho ya upinzani. Msafara wa mabasi umejaribu kuwaondoa raia zaidi leo kutoka mjini humo.
Gavana wa eneo la Donetsk amesema mashambulizi ya Urusi yamewaua watu 21 jana Jumanne, idadi inayoelezwa kuwa kubwa tangu vifo vilviyotokea Aprli 8, wakati shambulizi kwenye kituo cha treni huko Kramatorsk liliwpoaua watu wapatao 59.
Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amenukuliwa na shirika la habari la RIA akitahadharisha kuwa jeshi la nchi hiyo litayishambulia na kuyaharibu magari ya jumuiya ya NATO yanayosafirisha silaha Ukraine.
reuters, ap, afp