1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wataka mkutano maalum wa wahamiaji

30 Agosti 2015

Mawaziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani,Ufaransa na Uingereza Jumapili (30.08.2015)wataka kuitishwa mkutano maalum wa mawaziri wote 28 wa nchi za Umoja wa Ulaya kujadili mzozo wa sasa wa wahamiaji wanaoingia Ulaya.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere.Picha: picture-alliance/dpa/E. Laurent

Mawaziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani,Ufaransa na Uingereza Jumapili (30.08.2015)wametowa wito wa kuitishwa mkutano maalum wa mawaziri wote 28 wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kujadili mzozo wa sasa wa wahamiaji wanaoingia Ulaya.

Umoja wa Ulaya unakabiliana na wimbi la wakimbizi wanaoingia Ulaya ambao haikuwahi kushuhudiwa tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.Wengi wao wanazikimbia nchi zilizokumbwa na vita kama vile Syria na Afghanistan na kuhatarisha maisha yao katika safari ngumu za kuwafikisha Ulaya magharibi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amekaririwa akisema " Sote tumekubaliana kwamba hatuwezi kupoteza muda zaidi. Hali iliopo hivi sasa inahitaji hatua ya haraka na mshikamano ndani ya Umoja wa Ulaya."

Katika taarifa ya pamoja na mwaziri wenzake wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneeuve na Theresa May wa Uingereza kufuatia mazungumzo yao ya Jumamosi wametowa wito kwa Luxembourg ambayo inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya kuitisha mkutano katika kipindi kisichozidi wiki mbili.

Mkutano ujao wa kawaida wa mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya umepangwa kufanyika tarehe nane Oktoba.

Kuanzishwa maeneo ya hatari

Mawaziri hao watatu pia wametowa wito wa kuanzishwa kwa haraka maeneo ya hatari kusajili na kuchukuwa alama za vidole na kuwajuwa wakimbizi wa kweli hali kadhalika kufikia makubaliano ya haraka ya orodha pana ya Umoja wa Ulaya juu ya nchi zinazotambulika kama salama ambapo kwayo wahamiaji wanaweza kurudishwa.

Waziri wa Mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve na mwenzake wa Uingereza Theresa May.Picha: Getty Images/AFP/L. Neal

Ugiriki hususan iko katika shinikizo kutokana na matatizo ya kiuchumi na imekuja kuwa kituo kinachopendwa kutumiwa na watu wanaojaribu kuingia Ulaya ya magharibi.

Repoti kutoka Ugiriki hapo Jumapili zimesema mhamiaji mwenye umri wa miaka 17 ameuwawa baada ya kunasa katika mashambuliano ya risasi kati ya polisi doria wa mipaka wa Umoja wa Ulaya na kundi la watu wanaosafirisha wahamiaji kwa magendo.

Tukio hilo limetokea karibu na kisiwa cha Ugiriki cha Symi wakati maafisa wa shirika la udhibiti wa mipaka ya Ulaya Frontex walipopambana na kujaribu kuwazuwiya watu wenye silaha waliokuwa wakiwasafarisha wahamiaji 60 kwa kutumia boti ya mwendo wa kasi.

Kuuwawa mhamiaji

Kwa mujibu wa repoti ambazo sio rasmi kutoka duru za walinzi wa mwambao kundi hilo lenye kusafirisha watu kwa magendo lilifyetulia risasi boti hiyo ya doria jambo lililopelekea majibizano ya risasi na kuzuiliwa kwa boti hiyo yenye wahamiaji ambapo watu watatu walikamatwa.

Wahamiaji wa Syria baada ya kuvuka kuingia Hungary kutoka mpaka wa Serbiá.Picha: Reuters/B. Szabo

Kijana aliyewawa alipatikana akiwa sehemu ya chini ya boti akiwa na jeraha la risasi.Kila siku feri za Ugiriki zinawaingiza nchini humo maelfu ya wahamiaji wengi wao wakiwa wanataka kuelekea magharibi mwa Ulaya kwa kutumia njia ya Balkan kupitia Macedonia na Serbia ilii kuingia upya Umoja wa Ulaya kwa kutokea Hungary.

Vyombo vya habari vya ndani ya nchi vimeripoti kwamba wahamiaji 4,000 wametolewa kwenye boti 100 nje ya kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos Jumamosi pekee.

Hungary ambayo imekamilisha kujenga uzio wake uliokosudia kuwazuwiya wahamiaji kuingia nchini humo kutoka Serbia hapo Jmamosi imeshutumiwa na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius ambaye amesema hatua hiyo haiendani na maadili ya Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa

Mhariri : Isaac Gamba