1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chanjo za Corona: Umoja wa Ulaya watangaza taratibu kali.

30 Januari 2021

Umoja wa Ulaya umetangaza taratibu kali kwa ajili ya kudhibiti mauzo ya chanjo za corona. Kulingana na taratibu hizo nchi za Umoja wa Ulaya zitakuwa na mamlaka ya kuzuia uuzaji wa chanjo hizo nje ya jumuiya hiyo. 

Israel Tel Aviv | Coronavirus | Impfstoff Pfizer-BioNTech
Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Taratibu hizo kali zinaweza kuathiri usafirishaji kwa mataifa kama Uingereza, hatua ambayo inaonekana kuuongeza mzozo kati ya Jumuia ya Ulaya na nchi hiyo kutokana na uhaba wa chanjo hizo za kuokoa maisha.

Ireland Kaskazini na Uingereza tayari zimeonesha wasiwasi kutokana ana hatua hiyo. Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson walifanya mazungumzo kwa njia ya simu wakati ambapo waziri mkuu wa Uingereza alielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya athari inayoweza kutokea.

Soma zaidi:WHO yazilaumu nchi tajiri kwa kujilimbikizia chanjo za COVID-19

Shirika la afya duniani WHO limeikosoa hatua hiyo lakini Umoja wa Ulaya umeeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha kwamba kampuni za madawa zinatekeleza mikataba iliyosainiwa.

Umoja wa Ulaya umesema utafuatilia na ikiwa itabidi utazuia kuuzwa kwa dawa hizo nje ya jumuiya hiyo. Uamuzi huo umesababishwa na mvutano kati ya Umoja wa Ulaya na kampuni ya madawa ya Uingereza na Sweden- AstraZeneca. Kampuni hiyo imesema haina uwezo wa kuiuzia Umoja wa Ulaya vichupa vya chanjo kwa mujibu wa mkataba wa uliofikiwa baina ya pande mbili hizo.

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der LeyenPicha: picture-alliance/dpa/T. Monasse

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Jumuiya ya Ulaya inatarajia kampuni ya dawa ya AstraZeneca kuheshimu mkataba na kutoa chanjo kwa wakati. Tume ya Ulaya imesema inahisi dozi za chanjo kwa ajili ya Jumuiya ya nchi za Umoja wa Ulaya kutoka kwenye kiwanda cha AstraZeneca kilichopo kwenye eneo la Umoja wa Ulaya zimesafirishwa kwenda Uingereza kinyemela. Jumuiya hiyo imeitaka Uingereza kuhakikisha kuwa Umoja wa Ulaya pia unanufaika na chanjo za kampuni hiyo kutoka kwenye viwanda vyake viwili viliyvopo nchini Uingereza kwa ajili ya watu wote wa bara Ulaya.

Rais wa tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema anatarajia kampuni hiyo itawasilisha dozi milioni 400 kama ilivyokubaliwa na kwamba Umoja wa Ulaya utaendelea kufanya kila uwezalo kupata chanjo kwa ajili ya bara zima la Ulaya, majirani na washirika wa Ulaya ulimwenguni kote.

Vyanzo:/AP/ https://p.dw.com/p/3obCy

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW