1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Umoja wa Ulaya watia neno mkataba wa Ethiopia na Somaliland

3 Januari 2024

Umoja wa Ulaya umesema uhuru wa Somalia unapaswa kuheshimiwa kwa kuzingatia katiba ya nchi hiyo pamoja na mkataba wa Umoja wa Afrika na ule wa Umoja wa Mataifa.

Raia wa Ethiopia huko Dire Dawa
Raia wa Ethiopia kwenye mji wa Dire Dawa wakiandamana kuunga mkono mkataba baina ya nchi hiyo na jimbo la Somalia la Somaliland.Picha: Mesay Tekelu/DW

Mwito huo unafuatia hatua ya Ethiopia ya kutia saini mkataba wenye utata na jimbo la Somalia lenye utawala wa ndani la Somaliland.

Mkataba wa makubaliano uliotiwa saini siku ya Jumatatu na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi, unaipa Ethiopia nafasi ya kuitumia bandari ya Berbara iliyopo kwenye Bahari ya Sham na kutumia pia kambi ya kijeshi iliyokodishwa.

Jana, Somalia iliapa kutetea eneo lake na kuyataja makubaliano hayo kati ya Ethiopia na Somaliland kuwa "uchokozi" huku ikimuita nyumbani balozi wake kutoka Ethiopia.

Somaliland yenye wakazi takriban milioni 4.5 imekuwa ikitaka kutambuliwa kama taifa huru tangu ilipojiengua  kutoka Somalia mnamo mwaka 1991.