Umoja wa Ulaya watofautina kuhusu msaada Ukraine
27 Oktoba 2023Akizungumza katika mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa ulaya mjini Brussels, wanaokutana kujadili bajeti ya Umoja huo kwa miaka minne ijayo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema anahisi wataafikiana kuhusu uthabiti wa kifedha akisema hadhani migawanyiko inayoonekana itaathiri hilo.
Awali Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Oban alisema haoni haja ya taifa lake kutumia fedha za walipa kodi kuisaidia Ukraine.
Pia Waziri Mkuu wa Slovakia Roberto Fico ameungana na Oban akisema haungi mkono tena Ukraine kupewa msaada ya kijeshi, akiongeza kuwa kile watakachochangia ni msaada tu wa kibinaadamu.
Soma pia:Hungary na Slovakia zapinga msaada wa kifedha kutolewa Ukraine
Kwengineko rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema asingelipenda kuona mkutano baina ya Viktor Oban na rais wa Urusi Vladimir Putin ukiudhoofisha Umoja wa Ulaya.
Amesema kile anachoomba kulingana na hali ilivyo, kusitumike mwanya wa kuwasiliana na kujadili mambo fulani na Urusi akisema hilo litauharibu umoja wao.
Orban alikosolewa na baadhi ya viongozi wenzake wa mataifa 27 yanayounda Umoja wa Ulaya, kwa kukutana na Putin nchini China mwezi huu, wakati Moscow ikiendelea na vita vyake nchini Ukraine huku Ulaya ikijaribu kuitenga.
Ulaya kutuliza mzozo wa Israel na Hamas?
Akiuzungumzia mzozo wa Mashariki ya Kati kati ya Hamas na Israel, Macron amesema mataifa kadhaa ya Ulaya yanaangalia uwezekano wa kuunda Muungano wa kibinaadamu kwa ajili ya Gaza.
Aliongeza kwamba kwa sasa mazungumzo yanaendelea kati ya Cyprus na Ugiriki kuhusiana na mpango huo.
Amesema Cyprus inaweza kutumika kama eneo la operesheni za kibinaadamu.
Macron amesema mapatano kwa ajili ya kupitisha misaada ya kibinaadamu ni muhimu ili kuwasaidia watu wa Gaza wanaopitia hali ngumu.
Amesema anatambua haki na uhalali wa Israel kupambana na magaidi akiongeza kuwa Ufaransa iko tayari kutoa msaada wake.
Soma pia:Ulaya yataka eneo salama la kibinaadamu kuundwa Gaza
Lakini ametahadharisha kuwa mzingiro katika eneo la Gaza, kuendelea na mashambulizi ya wote na uvamizi wa ardhini ni hatari kwa watu wa Gaza.
Ameweka wazi kwamba Ufaransa inataka kuwaondoa raia wakeharaka iwezekanavyo kutoka ukanda wa Gaza unaovurumishiwa mabomu kutoka Israel. Mpango huo unasimamiwa na mamlaka ya Palestina pamoja na Misri.
Macron amesema mataifa mengine ya Ulaya pia yanapanga kuchukua hatua sawa na yake kwa ushirikiano wa karibu na taifa lake.
Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amesema kuwa mazungumzo ndani ya mkutano huo juu ya kifungu kipya juu ya sheria ya fedha ni magumu.
Amesema Umoja huo unatumai kumaliza mazungumzo hayo kufikia mwishoni mwa Desemba.