Umoja wakubaliana kibano zaidi katika matumizi ya fedha
9 Desemba 2011Mwanadiplomasia mmoja amesema viongozi wa nchi 27 waliopo katika mkutano wa siku mbili mjini Brussels, huko Ubelgiji, wamekubaliana kuwepo kwa vikwazo vya moja kwa moja kwa wanachama wa umoja huo watakaofanya matumizi zaidi ya uwezo wao. Taifa husika litaweza kuepuka vikwazo hivyo pale tu ambapo robo tatu ya mataifa ya umoja huo yatapiga kura ya huruma. Imeripotiwa pia kwamba viongozi hao wametaka Mahakama ya Umoja wa Ulaya kukagua kama kanuni za bajeti za umoja wa huo zipo katika sheria za kila taifa. Pamoja na makubaliano ya kinadharia, viongozi hao bado hawajajadili namna ya utekelezaji wake. Kwa upande wake Ujerumani imeripotiwa kusisitiza kufanyika mabadiliko ya msingi katika mkataba wa Umoja wa Ulaya, wakati rais wa baraza la umoja huo Herman Van Rompuy anapendelea kufanyika mabadiliko madogo ya haraka ambayo hayatohitaji kuidhinishwa rasmi.