1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yamtetea mjumbe wake maalumu Sudan

Angela Mdungu
27 Mei 2023

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameshtushwa na barua ya mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, inayoripotiwa kumuomba ambadilishe mwakilishi maalumu wa UN nchini humo Volker Perthes.

UN-Generalsekretär Antonio Guterres
Picha: Selcuk Acar/AA/picture alliance

Kauli ya Guterres kupitia kwa msemaji wake Stephan Dujarric imesema kuwa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anafurahishwa na kazi inayofanywa na Perthes na kuwa bado ana imani kubwa kwa mwakilishi huyo. Taarifa ya Guterres imetolewa wakati mkuu wa jeshi rasmi Jenerali Al Burhani akiwa kwenye mzozo na aliyekuwa msaidizi wake katika, Mohammed Daglo anayeongoza kikosi maalumu cha wanajeshi cha RSF.

Vikosi hivyo hasimu vimeingia katika siku ya tano ya makubaliano ya kuweka chini silaha kwa muda wa wiki moja, yaliyosimamiwa na Marekani pamoja na Saudi Arabia. Licha ya makubaliano hayo, pande hizo hasimu zimekuwa zikituhumiana mara kwa mara kuyakiuka.

Hadi sasa, kati ya Jeshi la Sudan na Umoja wa Mataifa hakuna upande uliochapisha nakala rasmi za barua ya Burhani inayodaiwa kuwa imeomba kuondolewa kwa Perthes kama mwakilishi maalumu wa Guterres nchini humo. Kwa sasa, mwakilishi huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa yuko mjini New York alikotoa muhtasari kwa baraza la usalama mwanzoni mwa wiki juu ya hali ilivyo katika taifa hilo. Hakuna taarifa ni lini atarejea Khartoum ambako mamlaka hazijatoa viza kwa raia wa kigeni  tangu vita vilipoanza. 

Barua ya Burhani, ni mfululizo wa hatua zinazochukuliwa na mkuu huyo wa Jeshi ambapo wiki iliyopita alimfuta kazi Daglo kama msaidizi wake katika baraza linalotawala. Aliwavuta karibu watu wanaomuunga mkono kijeshi na sasa anafanya juhudi za kuimarisha safu za jeshi lake.

Soma zaidi:Marekani, Saudia wasema usitishwaji mapigano Sudan unaheshimiwa kwa kiwango fulani

Ijumaa, wizara ya ulinzi ya Sudan iliwataka wanajeshi wastaafu pamoja na watu wanaoweza kutumia silaha wafike katika kamandi za jeshi zilizo karibu nao, wachukue silaha ili wajilinde wao, familia zao na majirani. Baadaye, ilitolewa kauli ya kuwataka wanajeshi wa akiba na wanajeshi wastaafu pekee wajiunge na jeshi. 

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker PerthesPicha: ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images

Perthes na Ujumbe wa Umoja wa Umoja wa Mataifa nchini humo wamekuwa wakilengwa na maandamano ya maelfu ya wafuasi wa Kiislamu na wale wa jeshi wakimtuhumu mjumbe huyo kuwa kuingilia mambo ya ndani ambapo wamekuwa wakitaka aondolewe Sudan

Maandamano kama hayo yalifanyika katika mji ulio mashariki mwa nchi hiyo wa Port Sudan tangu ilipoanza vita  Aprili 15. Umoja wa mataifa unasema zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao na wengine 300,000 wamekimbilia kwenye mataifa jirani tangu kuanza kwa mzozo huo. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW