1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utamaduni

Umuhimu wa matamasha ya kiutamaduni katika jamii

17 Novemba 2025

Matamasha ya kitamaduni hayatoi burudani pekee, bali ni darasa lenye thamani kubwa kwa jamii. Kupitia matamasha haya jamii hujifunza asili yao, na vijana hupata nafasi ya kuelewa mizizi ya tamaduni zao.

Mtwara, Tanzania 2025 | Utamaduni na Sanaa | Kikundi cha ngoma cha Mnyahi
Akina mama wa Kimakonde wa kikundi cha Mnyahi, wakicheza ngoma ya SindimbaPicha: Salma Mkalibala/DW

Mkoani Mtwara, kusini mwa Tanzania, kila mwaka hufanyika Tamasha la Makuya linalosherehekea urithi wa makabila matatu makubwa ya mkoa huo ambao ni Wamakonde, Wamakua na Wayao, ambapo wasanii wa jadi huendeleza sanaa za asili ambazo zipo hatarini kusahaulika.

Makuya ni tamasha la wanajamii wa mkoa wa Mtwara, linalobeba historia, utambulisho na fahari ya watu wa kusini mwa Tanzania. Jina Makuya ni kifupi kinachowakilisha makabila ya Wamakonde, Wamakua na Wayao.

Juhudi za kutangaza utamaduni wa jamii za Mtwara

Makabila haya yameenea katika maeneo tofauti ya mkoa huu: Wamakonde wanapatikana Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini, Tandahimba na Newala; Wamakua wanapatikana zaidi wilayani Masasi; na Wayao katika wilaya ya Nanyumbu.

Tamasha la Makuya lilianzishwa mwaka 2014 na limekuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la kulinda, kuendeleza na kutangaza utamaduni wa wanajamii wa mkoa wa Mtwara, sambamba na kuzitangaza ngoma za asili na wasanii wa kitamaduni.

Saidi Chilumba, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ADEA ambayo ndio waandaji wa tamasha hilo, anasema waliona kwamba kuna haja ya kuanzisha tamasha la Makuya, ili wanajamii waendeleze mila na desturi zao, na waweze kurithisha kikazi kingine vitu ambavyo wanajamii walikuwa wanavifanya hasa wazee wao, kwa kuzingatia vitu ambavyo vilikuwa ni vizuri katika jamii. 

Kikundi cha ngoma ya Ngongoti wanatumia magongo marefu kutoa elimu kuhusu mila na desturi za tamaduni za WamakondePicha: Salma Mkalibala/DW

''Lakini pia ilikuwa ni kulinda utamaduni wa wanajamii wa mkoa wa Mtwara, hizi mila na hizi tamaduni za hawa wanajamii ziweze kulindwa kizazi hadi kizazi kupitia ngoma, hasa pale wanapoimba zile nyimbo. Kila nyimbo au kila kikundi cha ngoma kinakuwa na maana fulani katika jamii,'' alibainisha Chilumba.

Kupitia Tamasha la Makuya, mambo mbalimbali ya kitamaduni hupewa kipaumbele, ikiwemo maonesho ya asili yanayohusisha mtindo wa maisha, mavazi ya kiasili yaliyotumika enzi za kale kama yale yaliyotengenezwa kwa magome ya miti, ukindu, miyaa na kaniki. Maonesho ya vyakula vya asili, urembo wa kienyeji, vyombo vya muziki vya jadi, na kadhalika. Kulingana na Chilumba, tamasha hili limekuwa likichangia kulinda tamaduni za wanajamii wa mkoa wa Mtwara, kwani lina nafasi kubwa sana katika kuhifadhi au kulinda utamaduni wa wanajamii wa mkoa wa Mtwara.

Mpangilio wa tamasha

''Kwa sababu Tamasha la Makuya linajaribu kuwarudisha watu nyuma. Unapokuja kuangalia Tamasha la Makuya, utakuja kuona mpangilio wa ngoma jinsi ulivyo, lakini utaona mpangilio wa mavazi tunahakikisha haturuhusu wasanii kuvaa nguo ambazo sio za asili. Yaani unakuja kuona wasanii wamevaa nguo za magome, unakuja kuona wengine wamevaa magunia, ikiwa tu ni katika kuonesha kwamba ni kweli kuna watu ambao walikuwa wanaishi katika mazingira hayo,'' alibainisha Chilumba.

Zipo baadhi ya tamaduni ambazo zilianza kupotea, ikiwemo usimuliaji wa hadithi za kale, na sasa kupitia Tamasha la Makuya, wanatumia jukwaa hilo kuwapa nafasi viongozi wakuu wa makabila kama Mkurungwa wa Wamakonde, Mwenye wa Wayao na Mwenye wa Wamakua, kueleza simulizi na miiko iliyokuwa sehemu ya maisha ya jamii zao.

Vikundi mbalimbali vya ngoma kutoka wilaya zote za mkoa wa Mtwara huwa vinapata nafasi ya kushiriki katika tamasha hilo, miongoni mwao ni vikundi vya Chimbuko na Ngongoti kutoka kabila la Wamakonde. Wasanii Rukia Rashidi na Ismail Mohamed wanasema ushiriki wao ni fursa ya kuenzi utamaduni wao na kuutambulisha kwa vizazi vipya.

Wamakua na ngoma ya Namashambura, wanatumia vinyago vya wanyama kutoa elimu Picha: Salma Mkalibala/DW

''Ushiriki wetu kwenye Tamasha la Makuya umetuletea mafanikio ya kujenga urafiki na watu mbalimbali ambao tunakutana nao, kufahamiana nao na wengine kujenga ujamaa,'' alifafanua Ismail. Kwa upande wake Rukia anasema kuna faida fulani ambayo wanakutana nayo ya kukutana na vikundi vingine na ikachangia kujifunza tamaduni zao na wao wakaonesha utamaduni wao kwa faida ya watu wengine ambao wanakwenda kuliangalia tamasha hilo.

Mmoja wa watazamaji wa tamasha hilo, Mussa Nduli, amesema matukio kama hayo yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha umoja wa jamii na kuhamasisha vijana kujivunia utamaduni wao. Anasema kupitia tamasha hilo amekuwa akijifunza tamaduni za makabila mengine kupitia ngoma za asili ambazo zimekuwa zikitumbuiza.

Mafundisho mbalimbali kupitia tamasha

''Pia unajifunza hata baadhi ya lugha ama misemo ile ambayo imekuwa ikitumika na makabila mengine, inawezekana usijuwe sana Kimakua, lakini kupitia tamasha hili unaweza ukalitumia sasa ukajifunza hata salamu tu, ingawa naamini pia hata makabila mengine ambayo yamekuwa yakishiriki wanajifunza kama ambavyo sisi Wamakonde tunajifunza,'' alisema Nduli.

Tamasha la Makuya ni muhimu na kitovu katika kutangaza tamaduni ndani na nje ya nchi, kivutio cha utalii, ajira kwa wanajamii, jukwaa la urithi wa utamaduni na chuo cha burudani kwa kuwa jamii inajifunza kwamba utamaduni ni utajiri, na unapothaminiwa, unaweza kuwa chanzo cha uchumi, utalii na umoja wa kitaifa.