1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mlima Meru na faida zake kitamaduni

Veronica Natalis
13 Juni 2025

Mlima Meru ulipo Arusha kaskazini mwa Tanzania, una umuhimu mkubwa wa kitamaduni, na ni sehemu ya historia kwa watu wa kabila la Wameru.

Mlima Meru ulioko katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha
Mlima Meru ulioko katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha, TanzaniaPicha: Ramadhani Mvungi/DW

Mlima Meru ulioko ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha, unatambuliwa kama Mlima wa Volkano. Ni mlima wa pili kwa urefu nchini Tanzania baada ya Mlima Kilimanjaro na ni wa tano kwa urefu barani Afrika.

Pamoja na shughuli mbalimbali za kibinadamu zinazoendelea pembezoni mwa Mlima Meru kama vile kilimo na ufugaji, kabila la Wameru pamoja na jamii nyingine zinazouzunguka mlima huo, hufanya ibada maalumu pembezoni mwa mlima kama ishara ya kuenzi tamaduni zao, ikiwemo ibada kwa ajili ya kilimo.

Wameru wanaendelea kuenzi tamaduni zao

Jamii ya watu hao hufanya ibada hasa katika maeneo ya misitu, maporomoko ya maji na kwenye miti, maeneo ambayo yanauzunguka mlima huo. Alfred Mungai kutoka jamii ya Wameru, anasema bado wanaendelea kuenzi tamaduni zao na kwamba huwa wanaenda katika mlima huo kwa ajili ya kufanya ibada.

''Tuna tamaduni nyingi na ibada mbalimbali, kama tu yalivyo makabila mengine, bado tunaendeleza tamaduni za asili za mababu zetu. Tofauti na kufanya ibada kwa ajili ya kuomba baraka kwenye kilimo, huwa tunaombea pia mambo ya mahusiano, familia, uchumi na hali ya hewa,'' alifafanua Mungai.

Mlima Meru ukionekana katika mandhari ya kuvutiaPicha: Ramadhani Mvungi/DW

Mbali na shughuli za kitamaduni, lakini pia wakazi wanaozunguka mlima huo wameweza kufaidika kwa shughuli za kilimo. Musa Juma ni mfanyabiashara wa mbao, anasema yeye ni mnufaika wa moja kwa moja, kwani hupata miti ya mbao kando na mlima huo.

''Si mimi tu, bali vijana wengi wamenufaika, kando na mlima, kuna mashamba ya mazao kama mahindi viazi, karoti, lakini pia kuna miti ya mbao. Mimi ni mdau, huwa nafuata mbao kule,'' alibainisha Juma.

Matambiko hufanyika wakati wa majira ya mvua 

Wakati wa majira ya mvua jamii ya Wameru hufanya matambiko na sherehe zinazohusiana na mafanikio na umoja wa familia au kabila, ambazo mara nyingi husheheni ngoma, nyimbo na michoro ya asili inayotumika kuelezea matukio ya muhimu ya kijamii na kitamaduni.

 ''Nawasihi watu waendelee kuenzi tamaduni nzuri za makabila yao, kwani zinadumisha umoja na mshikamano,'' alisema Mungai.

Wameru huishi kwa kutegemea kilimo, na Mlima Meru huongeza faida yao kwa upatikanaji wa maji na udongo bora. Mlima huu umechangia sana katika maisha ya Wameru, kutokana na faida zake za kilimo hadi ibada zao.