Ujue umuhimu wa tiba sahihi ya mifupa
24 Novemba 2025
Mifupa ina umuhimu mkubwa kwenye umbo la binadamu na ndio hubeba mwili wenye misuli na mishipa mbalimbali. Mifupa husaidia viungo vingine kufanya kazi ipasavyo na kuusaidia pia mwili wa binaadamu kuweza kusimama imara, kutembea na kadhalika.
Lakini unafahamu kuwa, kutibu mifupa kwa njia zisizo sahihi kunaweza kuathiri afya yako na kupelekea kupoteza viungo au kupata ulemavu wa kudumu? Zifahamu hatari za matibabu ya kienyeji katika kuunganisha mifupa. Wataalamu wa magonjwa ya mifupa na majeraha wanaonya kuwa tiba zisizo sahihi za kuunganisha mifupa ni hatari kwa afya, kwani mara nyingi hazizingatii taratibu za kisayansi na hutegemea mbinu za kienyeji ambazo huongeza ukubwa wa tatizo kwa mgonjwa.
Kulingana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mifupa na Majeraha kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, Dkt. Lameck Moses, uungaji wa mifupa kwa njia za kienyeji umekuwa ukisababisha madhara makubwa kuliko faida. Anaeleza kuwa wagonjwa wengi wanaotumia tiba hizo huishia kupata maambukizi, kushambuliwa na bakteria, au kushindwa kupona majeraha yao ipasavyo.
"Miongoni mwa madhara ambayo yanatokea kwa kuunga mifupa kienyeji kwa wale ambao wamevunjika na mfupa kutokea nje au kupata michubuko ni kushambuliwa na bakteria kwenye misuli au mifupa, kuungwa vibaya kutokana na njia zinazotumika kutozingatia taratibu za kisayansi yani unakuta mtu amevunjika mfupa na unatakiwa unyooshwe labda uweke chuma lakini unawekwa mti au kuna dawa fulani inapakwa akiwa na imani kwamba unapona, matokeo yake baadaye anajiona kweli maumivu yale ya mwanzo hana, lakini ukiangalia kwenye X-ray au vipimo vingine kama CT-scan unakuta mfupa umepinda au kutonyooka kama inavyotakiwa, ” alisema Dkt.Moses.
Takwimu rasmi za serikali
Akiendela kueleza daktari huyo anasema madhara mengine ya tiba hizo ni pamoja na kuoza kwa viungo, jambo linaloweza kusababisha kupoteza mikono au miguu, ongezeko la idadi ya watu wenye ulemavu, muda mrefu wa kupona, utegemezi, mashambulio ya moyo, na hata kiharusi. Kwa hivyo, ni muhimu kukabiliana na ajali au jeraha lolote kwa haraka kwa kuhakikisha unapata matibabu sahihi kutoka kwa wataalamu hospitalini mara tu tatizo linapotokea.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya nchini Tanzania, majeraha ya mikono na miguu ni miongoni mwa matatizo yanayoathiri watu wengi, hali inayochangiwa zaidi na ajali za barabarani hususan zinazohusisha pikipiki chombo kinachotegemewa na wengi katika shughuli za kila siku. Lakini hata hivyo walio wengi hawapati matibabu yaliyo sahihi katika majeraha yao kutokana na kuwa na mitazamo potofu.
"Wengine uelewa wao mdogo, wengine wanahofia gharama au kutojuwa kabisa, wakati wengine wakiathiriwa na imani za kijadi ambazo zimeenea mtaani, kwa hiyo hilo ni tatizo kubwa sana ambalo lipo kwa sababu ni mara chache sana kuona mgonjwa ametibiwa kienyeji na amepona bila kupata athari yoyote katika eneo ambalo ametibiwa, lakini wagonjwa wengi wanaokuja hospitalini wakiwa tayari wamepata madhara, ” alifafanua daktari Moses.
Ushuhuda wa walioathirika
Michael John ni kijana anayeishi wilayani Masasi hapa mkoani Mtwara, alipata ajali ya pikipiki na kuvunjika bega la mkono wake wa kulia, aliamua kutibiwa kwa mganga wa kienyeji kabla ya kwenda hospitalini.
"Nilipata ajali ya pikipiki mwaka jana, bega langu la mkono wa kulia liliumia vibaya. Marafiki zangu wakaniambia kuna mtu anajua "kuunganisha mifupa” kienyeji. Nilienda huko, akaweka dawa za majani na kuniwekea miti ya mianzi. Nilikaa zaidi ya wiki tatu, maumivu yakazidi na mkono ukaanza kuvimba na kutoa usaha. Nilipopelekwa hospitali, daktari alisema mifupa ilikuwa imeunganishwa vibaya na nilitakiwa kuungwa upya. Nilipitia maumivu makali sana. Na hadi leo mkono wangu hauwezi kufanya kazi kama zamani, ”alisema kijana huyo.
Michael anasema anajutia maamuzi aliyoyafanya, akieleza kuwa kama angewahi kwenda hospitalini huenda angepona mapema na kurejea kwenye shughuli zake za kila siku, badala ya kupitia changamoto na mateso anayokabiliana nayo sasa.
Wito wa wataalamu wa afya
Daktari Lameck Moses ametoa wito kwa wanajamii kuepuka tiba za kienyeji, akisisitiza kuwa majeraha ya mifupa yanapaswa kutibiwa hospitalini na wataalamu waliobobea.
"Wanapopata majeraha yoyote, wakimbilie hospitalini kwanza ili wajue hatma ya tatizo lake lipoje na litashughulikiweje, ili baadaye asije akapata madhara makubwa na kumfanya akose raha ya maisha au mwingine apoteze kiungo au apate adha ya matibabu ya muda mrefu, kumbe angeenda hospitalini huenda angepata huduma hiyo kwa haraka zaidi tu na asingekaa kwa muda mrefu, ”alisisitiza Dkt.Lameck Moses.
Kwa ujumla, wataalamu wanasisitiza kuwa afya ya mifupa ni jambo nyeti linalohitaji uangalizi wa kitaalamu. Jamii inakumbushwa kuachana na imani potofu na tiba za kienyeji, kwani kufanya hivyo kutasaidia kuokoa viungo, kupunguza ulemavu, na kulinda afya kwa ujumla.