UN: China huenda ilitenda uhalifu dhidi ya binadamu Xinjiang
1 Septemba 2022Ripoti hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu imebainisha kwa kina msururu wa ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya watu wa jamii ya Uyghurs na jamii nyingine ndogo za Waislamu katika mkoa wa Xinjiang ulioko magharibi mwa China. Ripoti hiyo hata hivyo haikutaja mauaji ya kimbari, mojawapo ya madai yaliyotolewa na Marekani na wakosoaji wengine.
China yawafundisha Waighuru propaganda kambini kwa lazimaMkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, ambaye amekabiliwa na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya wanadiplomasia na makundi ya haki za binadamu kwa msimamo laini dhidi ya China, aliwasilisha ripoti hiyo, dakika chache kabla ya muhula wake wa miaka minne kumalizika jana Jumatano. Sehemu ya ripoti hiyo inasema; "ukamataji wa kiholela na wa kibaguzi dhidi ya watu wa jamii ya Uyghur na Waislamu wengine katika mkoa wa Xinjiang nchini China, unaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu".
Aidha, ripoti hiyo ndefu yenye takribani kurasa 48 imeeleza kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mkoa wa Xinjiang unaofanywa na serikali ya China katika muktadha wa kukabiliana na ugaidi na itikadi kali.
Umoja wa Mataifa ulipaswa kuchapisha ripoti hiyo mwaka jana lakini ilicheleweshwa kwasababu mkuu wa ofisi ya haki za binadamu alikuwa katika mazungumzo ya miezi kadhaa na serikali ya China juu ya kuruhusiwa kuitembelea nchi hiyo.
Miongoni mwa mambo mengine yalibainishwa ni "mifumo ya mateso'' ndani ya kile Beijing inakitaja kuwa vituo vya ufundi stadi, ambavyo vilikuwa sehemu ya mpango wake wa kukuza maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza siku ya Jumatano baada ya ofisi ya Bachelet kutangaza kutoa ripoti hiyo, balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun, alisema Beijing "inapinga vikali" tathmini hiyo ya haki za binadamu.
"Tumeweka wazi kwa kamishna mkuu kwamba tunapinga vikali ripoti kama hiyo. Sote tunajua vizuri kwamba suala linaloitwa Xinjiang ni uwongo uliotungwa kabisa kwa sababu za kisiasa na lengo ni kudhoofisha utulivu wa China na kuzuia maendeleo ya China".
Mashirika ya haki za binadamu yanaishutumu Beijing kwa unyanyasaji dhidi ya watu wa jamii ya Uyghurs, na jamii nyingine ndogo za Kiislamu ambao wanafikia karibu milioni 10 katika mkoa wa magharibi wa Xinjiang. Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya China kuchukua hatua za haraka kuwaachia huru watu wote wanaozuiliwa katika vituo vya mafunzo, magereza au vituo vya vizuizi.