1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Dunia hatarini kutokana na mawimbi ya joto

20 Machi 2024

Umoja wa Mataifa umesema kuwa viwango vya joto duniani vilivunja rekodi mwaka uliopita,na kuonya kwamba mwaka huu wa 2024 huenda ukawa wa joto zaidi kuliko 2023.

Picha ya ishara Kuwait
Watu wakibarizi kwenye ufukwe wakati wa wimbi la joto katika mkoa wa Hawalii nchini Kuwait, Julai 20, 2023.Picha: Asad/Xinhua News Agency/picture alliance

Ripoti ya kila mwaka kuhusu hali ya tabianchi inayotolewa na Shirika la hali ya hewa la Umoja wa Mataifa, WMO, ilithibitisha data za awali zinazoonyesha kuwa mpaka sasa mwaka 2023 ndiyo wenye joto kali zaidi kuwa kurekodiwa.

Mkuu wa ufuatiliaji wa tabianchi wa WMO Omar Baddour, aliwambia wanadishi habari hapo jana kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaka huu wa 2024 utavunja rekodi ya 2023.

Maeneo kadhaa ya Ulaya yameshuhudia matukio ya moto wa misituni kutoka na wimbi la joto.Picha: DFES /AP/picture alliance

"Pia tayari tunarekodi kwamba Januari ilikuwa Januari yenye joto zaidi kwenye rekodi, kwa hivyo rekodi bado zinavunjwa, na hii kama unavyouliza, ni ishara gani? Kwa hivyo tayari tunazo dalili za kupitia mwaka wa joto sana wa 2024," alisema Baddour.

Akizungumzia ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alisema dunia ilikuwa kwenye kingo.  Katika hotuba yake kwa njia ya vidio, Katibu Mkuu Guterres alisema uchafuzi wa mazingira unaotokana na nishati za visukukuu unazidisha machafuko ya tabianchi, na kuonya kwamba mabadiliko yanaongeza kasi.

Hatari ya kupindukia nyuzi joto 1.5

WMO ilisema mwaka uliyopita kwamba wastani wa joto la uso wa dunia ilikuwa nyuzi 1.45 kwa kiwango cha Celsius juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya kiviwanda -- ikikaribia kiwango kinachotajwa kuwa hatari cha nyuzi joto 1.5, ambacho mataifa yalikubaliana kuepuka kukipita katika mkata wa Tabianchi uliofikiwa mjini Paris mwaka 2015.

Soma pia:Joto kali kwenye eneo la Arctic laongeza kitisho ulimwenguni 

Mkurugenzi Mkuu wa WMO Celeste Saulo, alitangaza kile alichokiita tahadhari ya hatari kuhusu hali ya tabianchi, akiwaambia waandishi habari kwamba mwaka 2023 umewwka rekodi mpya kwa kila kiashiria cha tabianchi.

Alisema ripoti hii ya kila mwaka inaonyesha kuwa mzozo wa tabianchi ndio changamoto inayowakabili wanadamu.

Mwanamke akienda kuchota maji kupoza kichwa chake wakati wa wimbi la joto nje ya Jacobabad, Pakistan.Picha: Akhtar Soomro/REUTERS

"Inafungamana kwa karibu na mzozo wa ukosefu wa usawa kama inavyoshuhudiwa na kuongezeka kwa uhaba wa chakula, uhamishaji wa watu na kutoweka kwa bioanuwaim" aliongeza.

Ugunduzi mmoja wa kutia wasiwasi hasa ulikuwa kwamba mawimbi ya joto ya bahari yalizikumba karibu theluthi moja ya bahari za dunia kwa wastani wa siku mwaka uliyopita.

Na kufukia mwishoni mwa 2023, zaidi ya asilimia 90 ya bahari zilikuwa zimeshuhudia wimbi la joto kwa wakati fulani katika mwaka huo, ilisema WMO, na kuonya kuwa joto kali la bahari husababisha madhara makubwa kwa mifumo ya ekolojia na matumbawe.

Chanzo: Mashirika