1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Dunia yahitaji sera salama za maji

19 Machi 2018

Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa watu bilioni 3.6, sawa na nusu ya idadi ya watu duniani, wanaishi katika maeneo ambayo huenda maji huwa kidogo angalau kwa mwezi mmoja kila mwaka.

Menschen holen Wasser mit Eimern, weil es bei ihnen zuhause kein fließendes Wasser gibt
Picha: DW/E. Boniphace

Umoja wa Mataifa unasema serikali duniani zinapaswa kuanzisha sera salama za kuimarisha usambazaji na ubora wa maji, wakati ambapo suala la mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la watu duniani vikitishia usalama na upatikanaji wa maji kwa mabilioni ya watu. Hayo ni kwa mujibu wa tamko la Umoja wa Mataifa wakati huu inapoanza wiki ya maji ulimwenguni.

Katika ripoti yake ya mwaka 2018 kuhusu maendeleo ya maji duniani ambayo imezinduliwa rasmi leo, Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa watu bilioni 3.6, hiyo ikiwa ni takriban nusu ya watu duniani kote, wanaishi katika maeneo ambayo huenda maji huwa kidogo angalau kwa mwezi mmoja kila mwaka.

Idadi ya wanaokosa maji kuongezeka hadi bilioni 5.7 ifikapo 2050

Ripoti hiyo imeonya kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia hadi watu bilioni 5.7 ifikapo mwaka 2050. Wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo nchini Brazil, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO,  Audrey Azoulay, amesema ripoti hiyo inapendekeza masuluhisho yanayoegemea utunzaji mazingira ili kushughulikia maji vyema na kuepuka migogoro ya maji.

Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaPicha: Reuters/United Photos/T. Kluiters

Wiki iliyopita wakati akikabidhiwa ripoti hiyo iliyoandaliwa na jopo lililowajumuisha wakuu wa nchi 11 na mjumbe maalum, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteres, alisema majanga yanayofungamana na maji yanazidi kuongezeka na kuwa hatari zaidi kila mahali. Hiyo inamaanisha suala la maji ni la kufa na kupona na hivyo ni lazima lipewe kipaumbele:

"Asilimia 60 ya miili yetu ni maji. Watu bilioni mbili duniani hawana maji salama na watu bilioni 4.5 hukosa mazingira safi, inamaanisha tunakabiliwa na changamoto kubwa."

Matumizi ya maji yameongezeka duniani

Ripoti hiyo imeeleza kuwa matumizi ya maji yameongezeka mara sita zaidi ikilinganishwa na karne iliyopita, na hali hiyo inazidi kuongezeka kwa kiwango cha asilimia moja kila mwaka. Hali hiyo imesababishwa na ongezeko la watu duniani, maendeleo ya kiuchumi na mabadiliko ya njia za matumizi ya maji miongoni mwa sababu nyinginezo.

Serikali zimehimizwa kutunga sera salama kuhusu maji ambazo ni rafiki kwa mazingiraPicha: DW/E. Boniphace

Mhariri mkuu wa ripoti hiyo, Richard Connor, amesema mbinu za zamani kama vile uchimbaji wa mabwawa ya maji kwa ajili ya umwagiliaji katika mashamba na ujenzi wa hifadhi nyinginezo haziwezi tena kutatua changamoto zilizoko.

Badala yake, ripoti imezidi kueleza kuwa mbinu za uhifadhi ambazo ni rafiki kwa mazingira mfano uhifadhi wa vyanzo vya maji, kuboresha viwango vya unyevunnyevu ardhini na kuongeza viwango vya maji yaliyomo chini ya ardhi zinaweza kuwa bora na nafuu zaidi.

Endapo mbinu hizo zikitumika, basi mazao ya kilimo yataongezeka kwa asilimia 20 duniani kote. Pia zitasaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo, ukame na mafuriko, huku zikiimarisha viwango vya misitu na ubora wa udongo, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: John Juma/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW