1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Guterres asikitishwa na mashambulizi ya Israel, Gaza

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
16 Mei 2021

Kwa mujibu wa msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, Guterres amefadhaishwa na idadi inayoongezeka ya vifo vya raia na majeruhi.

Israel Palästina Gazastreifen | Luftschläge in der Nacht
Picha: Mohammed Abed/AFP

Vurugu zinaendelea kati ya Israeli na kundi la Hamas linalotawala katika Ukanda wa Gaza hali inayosababisha wasiwasi katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea kusikitishwa kwake na mashambulio ya anga ya jeshi la Israel yaliyolenga na kuliharibu jengo la ghorofa 12 kwenye Ukanda wa Gaza. Jengo hilo lilikuwa na ofisi kadhaa za mashirika ya habari ya kimataifa na pia makazi ya watu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António GuterresPicha: Photoshot/picture alliance

Kwa mujibu wa msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, Guterres amefadhaishwa na idadi inayoongezeka ya vifo vya raia na majeruhi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza na kuzikumbusha pande zote kujiepusha na mashambulizi yanayowalenga raia na vyombo vya habari akisema yanakiuka sheria za kimataifa na kwamba ni lazima yaepukwe kwa kila hali.

Soma Zaidi:Shambulizi la Israel laporomosha jengo la ghorofa 12 Gaza

Ndege za kivita za Israeli zilipiga majengo kadhaa na barabara katika sehemu muhimu ya jiji la Gaza mapema siku ya Jumapili. Kulingana na picha zilizosambazwa na wakaazi wa eneo hilo pamoja na waandishi wa habari, mashambulio ya angani yamesababisha uharibifu mkubwa kwenye barabara kuu inayoelekea kwenye hospitali ya Shifa, ambayo ni kubwa zaidi kwenye Ukanda wa Gaza.

Taarifa ya wizara ya afya imefahamisha kwamba wengine wawili wameuawa kwenye mashambulio ya hivi karibuni ambapo pia watu 25 wamejeruhiwa, ikiwa ni pamoja na watoto na wanawake.

Wakati huo huo, nyumba ya kiongozi wa kundi la Hamas ilipigwa bomu Jumapili alfajiri na majeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza huku kundi hilo nalo likiripotiwa kufyatua makombora yaliyoelekezwa katika mji wa Tel Aviv. Kiongozi huyo Yehya Al-Sinwar, ameliongoza kisiasa na kijeshi kundi la wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2017.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Ahmed Gharabli/AFP

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema operesheni hii ya kijeshi itaendelea kwa muda mrefu kadri itakavyohitajika.

Wanamgambo wa Palestina wamerusha makombora yasiyopungua 2,300 kuyaelekeza nchini Israeli. Watu wapatao 10 wameuawa ikiwa ni pamoja na mtoto na mwanajeshi mmoja wa Israel. Zaidi ya Waisraeli 560 wamejeruhiwa.

Mashambulio mengine ya anga ya mapema Jumapili, yamesababisha kifo cha daktari mmoja mtaalamu katika Ukanda wa Gaza ambapo mkewe na binti yake walijeruhiwa.

Soma Zaidi:Zaidi ya Wapalestina 130, Waisraeli 9 wauawa

Uhasama kati ya pande hizo mbili unaongezeka na mashambulio yameingia katika siku ya saba bila ishara ya kupungua.

Wakati ambapo wajumbe kutoka Marekani, Umoja wa Mataifa na Misri wanaendelea na mazungumzo juu ya kurudisha utulivu, bado mpaka sasa hakuna dalili zinazoonesha maendeleo. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana baade Jumapili kuujadili mzozo kati ya Israel na Palestina.

Waandamanaji jijini London, Uingereza wapinga mashambulio ya GazaPicha: Tolga Akmen/AFP/Getty Images

Naye waziri wa Marekani anayeshughulikia mambo ya Israel na Palestina, Hady Amr anatarajiwa kufanya mazungumzo siku ya Jumapili na viongozi wa Israeli kabla ya kukutana na maafisa wa mamlaka ya Palestina kutafuta njia ya kurejesha hali ya utulivu na amani, hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Kwingineko maandamano yamefaynika kwenye miji mbalimbali duniani kupinga mashambulio ya anga ya Israel katika Ukanda wa Gaza. Waandamanaji wanaowaunga mkono Wapalestina waliingia mabarabarani katika miji ya Los Angeles, New York, Boston, Philadelphia na miji mingine ya Marekani. Maandamano mengine yalifanyika katika miji ya Berlinna Leipzig nchini Ujerumani na London nchini Uingereza.

 

Vyanzo: RTRE/AFP/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW