UN inatumai raia wa Congo watapiga kura kwa amani
23 Desemba 2018Raia wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo walipaswa kuelekea katika vituo vya kupigia kura hii leo Jumapili kumchagua rais wao, wabunge na viongozi wengine wa mikoa kabla ya uchaguzi huo kuahirishwa siku ya Alhamisi, na tume ya uchaguzi CENI ikisema moto katika ghala moja mjini Kinshasa, uliharibu mashine za kupigia kura.
Uchaguzi uliokuwa ufanyike 23.12.18 katika taifa hilo linalokumbwa na migogoro ya mara kwa mara ulitazamwa kama njia ya kusuluhisha mgogoro wa kisiasa wa miaka miwili kuhusu mustakabali wa rais Joseph Kabila.
Kulingana na taarifa ya nchi wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wanamatumaini kwamba kuahirishwa kwa uchaguzi kutatoa nafasi ya kuwa na mazingira bora kwa raia wa Congo kujieleza kwa uhuru mnamo Desemba 30 siku uchaguzi huo uliopangiwa kufanyika.
Baraza hilo pia limevitolea mwito vyama vyote vya kisiasa nchini humo kushiriki kwa amani na kwa ufanisi katika zoezi la uchaguzi ili kuhakikisha hatua ya kukabidhi madaraka inafanyika kulingana na katiba ya Congo na makubaliano ya Desemba mwaka 2016.
Uchaguzi, njia ya kusuluhisha mgogoro wa kisiasa kuhusu mustakabali wa rais Kabila.
Rais Joseph Kabila aliye na miaka 47 alitarajiwa kumaliza kipindi chake cha uongozi mwishoni mwa mwaka 2016 baada ya kumalizika mihula yake miwili ya uongozi kulingana na katiba ya taifa hilo aliendelea kuwepo kama msimamizi wa serikali jambo linalokubalika kikatiba. Uchaguzi ukaahirishwa hadi mwishoni mwa mwaka 2017 chini ya makubaliano ya kanisa lililo na nguvu la kikatoliki.
Kisha baadae ukaahirishwa tena hadi mwaka 2018 ambapo kabila hatimae alithibitisha kwambahatogombea tena uchaguzi. Kucheleweshwa kwa uchaguzi kwa miaka miwili kulisababisha vurugu na shinikizo la kufanyika uchaguzi kutoka kwa Mataifa ya Magharibi na Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa hiyo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limerejelea tena utayari wa MONUSCO, Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kusaidia wakati wowote iwapo wataombwa kufanya hivyo. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema mara kadhaa kwamba inataka kupanga uchaguzi wake bila usaidizi wa kifedha wala usaidizi wa vifaa kutoka kwa Umoja wa Ulaya au Umoja wa Mataifa.
Watu takriban milioni 46 wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi wa Desemba 30.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Iddi Ssesanga