1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIran

UN: Iran bado inawanyonga wahusika wa maandamano

5 Julai 2023

Ujumbe maalum wa Umoja wa Mataifa wa kuchunguza ukweli kuhusu kilichotokea nchini Iran, umesema nchi hiyo bado inatoa adhabu kali dhidi ya watu wanaoshukiwa kuhusika kwenye maandamano ya umma.

Maandamano I Iran
Maandamano ya kupinga wanaume wawili walionyongwa IranPicha: Allison Bailey/NurPhoto/picture alliance

Mnamo mwezi Novemba mwaka jana baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kuunda timu ya maafisa wa ngazi za juu waliopewa jukumu la kuchunguza kilichotokea katika kuwaandama waandamanaji nchini Iran.

Timu hiyo hivi sasa imekuja na matokeo ya uchunguzi wake,ambao unaonesha kwamba Iran bado inatowa adhabu kali kabisa kwa watu wanaoshukiwa walishiriki kwenye maandamano hayo dhidi ya serikali ya mjini Tehran. 

Mwenyekiti wa ujumbe huo,wa timu huru ya kimataifa ya kutafuta ukweli kuhusu kilichotokea nchini Iran, Sara Hossain akiripoti mbele ya baaraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa amesema miezi 10 tangu kifo cha  kijana Amin nchini Iran,bado familia yake haijapata haki ya kuujuwa ukweli na haki haijatekelezwa.

Sara Hossain ameongeza kusema kwamba ,kukosekana uwazi katika hatua nzima ya uchunguzi wa kifo cha kijana huyo wa kike kumejionesha wazi kufuatia hatua ya kukamatwa na kuendelea kushikiliwa rumande waandishi wawili wakike ,Nilufar Hamedi na Elahe Mohammadi.

Maandamano makubwa yaliyoikumba IranPicha: NNSRoj

Amesema serikali ya Iran imeshindwa kutowa ushirikiana na timu hiyo ya uchunguzi.

''Tumekabiliwa na changamoto kadhaa,na Kwanza ni kushindwa kuingia Iran kwasababu kuna sehemu kubwa ya watu tunaotaka kuzungumza nao na maeneo tunayotaka kuyatazama. Na vitu tunavyohitaji kuviangalia vipo ndani ya Iran. Kwahivyo kukosekana ushirikiano mpaka sasa ni changamoto kubwa sana.''

Iran ilikumbwa na maandamano makubwakabisa yaliyochochewa na kifo cha msichana Mahsa Amin mwenye umri wa miaka 22 mnamo mwezi Septemba mwaka jana, mwenye asili ya Kikurdi, aliyekamatwa kwa madai ya kukiuka maadili kwa kutovaa vizuri vazi la Hijabu kwa mujibu wa sharia ya kiislamu.

Watu chungunzima waliuwawa lakini pia wengi walikamatwa. Iran ilisema watu 22,000 waliokuwa wamekamatwa kuhusiana na maandamanohayo walipewa msamaha,lakini Hossain anasema tamko hilo linamaanisha kuna Wairan wengi ambao bado wanashikilia rumande au walioshtakiwa.

Kwa mujibu wa Hossain hakuna taarifa au data rasmi kuhusu mazingira ya tuhuma zinazowakabili wanaoshikiliwa au walioshtakiwa kuhusiana na maandamano hayo.

Mwenyekiti huyo wa ujumbe wa uchunguzi wa kimataifa kuhusu haki za binadamu anasema wengi waliosamehewa iliripotiwa kwamba walilazimishwa kukiri makosa na kutakiwa kusaini nyaraka ya kuahidi siku za baadae kutorudia kile kilichoitwa uhalifu walioufanya.

Picha ya msichana Mahsa Amin aliyefariki mikononi mwa polisi nchini IranPicha: Thibault Savary/Le Pictorium/MAXPPP/picture alliance

Lakini pia Hossain amebaini kwamba Iran inaendelea kutekeleza adhabu kali dhidi ya wale walishiriki maandamano ikiwemo kunyonga. 

Soma zaidi kuhusu hilo: Amnesty laishutumu Iran kwa kuwanyonga watu 173

Anasema kinachotisha zaidi ni kwamba watu 7 wanaume tayari wameshanyongwa baada ya kuhukumiwa kufuatia mchakato usioelewaka,usiokuwa na uwazi, uliotawaliwa na madai ya kutozingatia usawa,ikiwemo kulazimishwa kukiri makosa chini ya mateso makubwa.

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umeitaka Iran iachana na adhabu hiyo ya kuwanyonga watu waliohukumiwa kifo wakihusishwa na maandamano. Lakini pia wameitolea mwito serikali hiyo ya mjini Tehran kuwaachia wote inaowashikilia kufuatia maandamano hayo na itoe ushirikiano ya timu hiyo ya uchunguzi.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW