1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN:Juhudi za kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030 zinasuasua

22 Julai 2024

Umoja wa Mataifa umesema maamuzi ya kisiasa yatakayochukuliwa mwaka huu, yataamua ikiwa lengo la kutokomeza kabisa ugonjwa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030 linaweza kufikiwa.

Munich - Mkutano wa 25 wa Kimataifa wa kujadili ugonjwa wa UKIMWI
Kunakofanyika mkutano wa 25 wa Kimataifa wa kujadili ugonjwa wa UKIMWI uliofunguliwa rasmi siku ya Jumatatu (22.07.2024) mjini Munich, Ujerumani.Picha: Sabine Dobel/dpa/picture alliance

Kauli hiyo ya Umoja wa Mataifa imetolewa kwenye mkutano wa 25 wa Kimataifa wa kujadili gonjwa la UKIMWI uliofunguliwa rasmi siku ya Jumatatu mjini Munich, Ujerumani.

Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha kupungua kwa idadi ya vifo na maambukizi mapya pamoja na uboreshaji wa upatikanaji wa matibabu kwa wagonjwa walio na Virusi Vya Ukimwi (VVU). Lakini wakati takwimu hizo zikionekana kuwa chanya, shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS limeonya kuwa maendeleo jumla bado si ya kuridhisha sana.

Soma pia: Ukimwi - Kujikinga dhidi ya gonjwa hili

Ripoti ya shirika hilo imebainisha kuwa maamuzi yatakayochukuliwa na viongozi mwaka huu yataamua iwapo nchi zinaweza kufikia lengo la kuufanya UKIMWI kutokuwa tena tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030 na kuhakikisha maendeleo zaidi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Dawa za kupunguza makali ya Virusi Vya UkimwiPicha: Jens Kalaene/dpa/picture alliance

Katika kipindi cha zaidi ya miongo minne tangu kuibuka kwa janga hilo duniani kote, UKIMWI tayari umeua zaidi ya watu milioni 42. Licha ya idadi ya vifo kupungua kutoka watu 670,000 mwaka 2022 hadi 630,000 mwaka jana, idadi hiyo hata hivyo bado ni kubwa mno.

UNAIDS yahimiza kuchukuliwa kwa hatua zaidi

Mkuu wa shirika la UNAIDS Winnie Byanyima amesema katika ripoti hiyo kwamba kila dakika, mtu mmoja hufa kutokana na magonjwa yanayohusiana au kusababishwa na UKIMWI, huku akionya kwamba dunia inasuasua kufikia malengo makubwa ya kutokomeza  UKIMWI ifikapo mwaka 2030. Aidha Bi Byanyima amelitaka shirika linalotengeneza dawa za kupunguza makali ya VVU la Gilead kuzalisha zaidi dawa yake aina ya Lenacapavir ambayo inonyesha matokeo bora zaidi:

" Nadhani Gilead inayo fursa ya kutusaidia pakubwa kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma. Wanaweza kuweka historia kwa hilo, si tu kwa kuisambaza kote ulimwenguni kama dawa ya kuzuia maambukizi, lakini kwa kuruhusu matumizi yake kwa kila mtu na si tu kwa ajili ya kuzuia bali pia itumiwe kwa matibabu."

Mwenye VVU atahitaji sindano mbili tu kwa mwaka za dawa hiyo mpya ya Lenacapavir.

Mkuu wa shirika la UNAIDS Winnie ByanyimaPicha: Ryan Remiorz/Zuma/IMAGO

Mkuu huyo wa UNAIDS amesisitiza kuwa ukosefu wa usawa katika mapambano dhidi ya VVU haushughulikiwi vya kutosha, hasa ikizingatiwa kuwa dawa zenye ufanisi mkubwa zimekuwa zikiuzwa kwa bei kubwa.

Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 40 wanaishi na VVU , virusi ambavyo vinaweza kusababisha ugonjwa wa UKIMWI. Takriban maambukizi mapya milioni 1.3 yalirekodiwa mwaka jana. Upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU pia umeboreshwa, lakini bado ni suala tete.

Soma pia: Madaktari: Mtu wa saba huenda ´amepona´ virusi vya UKIMWI

Mwaka jana, watu milioni 30.7 walipata matibabu hayo ikilinganishwa na milioni 7.7 tu mwaka 2010. Lakini bado kuna changamoto nyingi ili kufikia lengo la kutokomeza kabisa UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Mashariki na kusini mwa Afrika yanasalia kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi, kwa kujumuisha vifo 260,000,  watu milioni 20.8 wakiwa wanaishi na VVU, na pia watu 450,000 wakiwa waliambukizwa virusi hivyo mwaka jana.

(Chanzo: AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW