Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laahirisha mkutano DRC
8 Januari 2019Kikao cha baraza hilo la usalama ambacho awali kilipangwa kufanyika leo Jumanne, kimeahirishwa hadi Ijumaa tarehe 11 mwezi huu wa Januari, baada ya maafisa wa Congo kuahirisha kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa Desemba 30. Matokeo hayo yalitarajiwa kutangazwa Jumapili iliyopita tarehe 6 mwezi huu. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa likifuatilia uchaguzi katika nchi hiyo ambapo umoja huo unaendeleza mojawapo ya oparesheni zake kubwa za kulinda Amani.
Baadhi ya mabalozi wanasema kumekuwepo tofauti kubwa katika baraza hilo kuhusu kutumwa kwa ujumbe wa pamoja wa uchaguzi huo wa Desemba 30 mwaka 2018. Kikao cha faragha kilichoandaliwa Ijumaa wiki iliyopita kwa saa mbili hakikufaulu kupata taarifa ya pamoja. Katika mkutano huo, Ufaransa ambayo iliitisha mkutano wenyewe ililitaka kundi hilo kutoa taarifa ya pamoja kuhusu umuhimu wa uchaguzi na matokeo.
Kulingana na wanadiplomasia wawili wa baraza hilo ambao hawakutaka majina yao kutajwa wamewaeleza waandishi wa habari kwamba mataifa mengine ikiwemo Afrika Kusini yanafikiri kwamba baraza hilo halifai kutoa tamko hadi matokeo yatakapojulikana. Huku hayo yakijiri, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress, Stephane Dujarric, amesema kwamba Umoja wa Mataifa una matumaini matokeo ya awali ya uchaguzi wa Congo yatatangazwa kwa wakati ufaao.
Dujarric pia amemkumbusha kila mmoja aliyehusika katika uchaguzi huo kuheshimu sheria za uchaguzi za Congo na kusaidia kudumisha mazingira yasiyokuwa na ghasia. Uchaguzi huo huenda ukaashiria mwanzo wa mabadiliko ya uongozi kwa njia ya demokrasia na Amani tangu Congo kujinyakulia uhuru mwaka 1960.
Rais wa muda mrefu Joseph Kabila alikuwa tayari ameahirisha uchaguzi huo kwa miaka miwili na baadhi ya raia wa Congo wana wasiwasi kwamba matokeo yanaweza yakabadilishwa ili kuhakikisha chama chake kinasalia uongozini kufuatia kucheleweshwa kutangazwa kwa mshindi wa uchaguzi huo.
Maafisa wa uchaguzi walisema Jumapili kwamba hakuna taarifa zozote zotakazotolewa hadi kura zote zitakapohesabiwa. Hata hivyo hawakutoa tarehe ya lini hilo litafanyika. Wakati huo huo, serikali imekatiza mawasiliano ya Intaneti kwa kile inachosema ni kuzuia uvumi kusambazwa kuhusu nani aliyeshinda.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE
Mhariri: Caro Robi