UN: Korea Kaskazini inaendelea na mpango wake wa Nyuklia
4 Agosti 2018Katika ripoti ya kurasa 62 iliyotumwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jopo la wataalam wa Umoja wa Mataifa pia limeorodhesha kukiukwa kwa vikwazo vya kuuza katika nchi za nje makaa ya mawe, chuma, vyakula vya baharini na bidhaa nyenginezo iashara zinazoiletea mamilioni ya dola utawala wa Kim Jong Un.
Ripoti hiyo imesema kuhamishwa kwa bidhaa za petroli katika meli za mafuta za Korea Kaskazini ndilo jambo linalosalia kuwa njia "kuu ya kukwepa vikwazo" ambapo meli 40 zinahusika pamoja na makampuni 130. Inasema pia ukiukaji huo umepelekea vikwazo vya hivi majuzi kutokuwa na athari yoyote.
Katika mkutano wa kilele wa kihistoria mwezi Juni huko Singapore pamoja na Rais wa Marekani Donald Trump, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alitia saini akubaliano ya kuziharibu silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea kwa matumaini ya kupata kuondolewa vikwazo na Umoja wa Mataifa na Marekani.
Korea Kaskazini ilijaribu kuuza silaha ndogondogo pia
Trump lakini ameionya Korea Kaskazini kwamba vikwazo ni lazima visalie na kuna uwezekano wa kuvikwazo hivyo kuwa vikali zaidi iwapo hakuna juhudi za taifa hilo kusitisha mpango wake wa nyuklia.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa pia imesema Korea Kaskazini pia ilijaribu kuuza silaha ndogondogo na vifaa vyengine vya kijeshi kwa Libya, Yemen na Sudan kupitia washenga wa kigeni.
Huku hayo yakijiri Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amezionya Urusi, China na nchi zengine dhidi ya kukiuka kwa aina yoyote kwa vikwazo vya kimataifa vya Korea Kaskazini hatua ambayo huenda ikapunguza shinikizo la Korea Kaskazini kuacha silaha zake za nyuklia.
Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa usalama wa mataifa ya bara Asia huko Singapore, Pompeo amewaambia waandishi wa habari kwamba Marekani ina ripoti mpya na za kuaminika kwamba Urusi inakiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa Korea Kaskazini kwa kukubali kufanya biashara na nchi hiyo na pia kutoa vibali vipya vya kufanyia kazi kwa wafanyakazi wa Korea Kaskazini.
Urusi na nchi zote lazima zitii maamuzi ya Umoja wa Mataifa
"Iwapo ripoti hizi zitaonekana kuwa sahihi, na tuna kila sababu ya kuamini kwamba ziko sahihi, huo utakuwa ni ukiukaji," alisema Pompreo. Waziri huyo wa Marekani amesema kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura na kukubaliana kwa pamoja kuhusu vikwazo hivyo.
"Tunataraji Urusi na nchi zote zitii maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuweka vikwazo kwa Korea Kaskazini," alisema Pompeo, "Ukiukaji wowote ambao unakwenda kinyume na lengo la dunia la kuziharibu silaha za nyuklia za Korea Kaskazini, ni kitu ambacho Marekani itakiangalia kwa umuhimu mkubwa sana," aliongeza Waziri huyo.
Mapema Jumamosi katika mahojiano na kituo cha habari cha Singapore Chanel News Asia, Pompeo alisema kasi ya kuziharibu silaha za nyuklia za Korea Kaskazini itategemea na Kim mwenyewe. Ila katika kikao na wanahabari, Pompeo ameonekana kurudi nyuma katika kauli hiyo akisema muda wa kuharibu silaha hizo utajadiliwa na Marekani na Korea Kaskazini.
Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE
Mhariri: Lilian Mtono