1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kupiga kura kuhusu mageuzi ya kura ya turufu

26 Aprili 2022

Nchi 193 wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa watapiga kura kuhusu azimio litakalowahitaji wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama katika siku za usoni kufafanua ni kwa nini wanaitumia kura yao ya turufu

Tunesien Tunis | Parlament
Picha: Fethi Belaid/AFP/Getty Images

Majadiliano ya mageuzi ya kura ya turufu ni nadra na yenye utata, lakini yamefufuliwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Huku ikizilenga moja kwa moja Marekani, China, Urusi, Ufaransa na Uingereza – ambao ndio pekee walio na haki ya kura ya turufu – hatua hiyo itawafanya kulipia gharama kubwa kisiasa wakati wakiamua kuitumia kura hiyo kulipinga azimio la Baraza la Usalama, amesema balozi mmoja wa nchi ambayo haina kura ya turufu na ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Wakosoaji wanaiita hatua hiyo, iliyowasilishwa na Liechtenstein, kuwa ni mageuzi rahisi ya kiutaratibu.” Lakini haijawa wazi kama mageuzi hayo yatawashinikiza wanachama hao watano wa kudumu kutoitumia sana kura yao ya turufu, au kama itatengeneza mazingira ya kutumiwa zaidi kura hiyo wakati wanachama wa kudumu wanapopendekeza rasimu zenye utata wanazofahamu kuwa wapinzani wao watazipinga ili wawalazimu kueleza hadharani ni kwa nini wakauchukua msimamo wao.

Urusi iliivamia kijeshi Ukraine Februari 24, 2022Picha: Sefa Karacan/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa rasimu hiyo, azimio hilo linalihitaji Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa kuandaliwa katika siku kumi za kazi baada ya mwanachama wa kudumu kutumia kura ya turufu kuijadili hali ambayo ilisababisha kura hiyo kutumika. Nchi 60 zimejiunga na Liechtenstein katika kuunga mkono mageuzi hayo, ikiwemo Marekani.

Uingereza na Ufaransa zitayapigia kura mageuzi hayo, hata ingawa zilijiepusha kuwa wafadhili wenza wa muswada huo. Urusi na China pia sio miongoni mwa walioifadhili rasimu hiyo. Mwanadiplomasia kutoka moja ya nchi hizo mbili, ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameikosoa hatua hiyo akisema "itaugawanya” Umoja wa Mataifa hata Zaidi.

Balozi wa Liechtenstein Christian Wenaweser amesema hatua hiyo itatengeneza utaratibu mpya akisisitiza kuwa pendekezo hilo "sio dhidi ya nchi yeyote.” Amesema halijaelekezwa dhidi Urusi, licha ya ukweli kwamba limekuwa likisubiri kwa Zaidi ya miaka miwili na kufufuliwa kwake kumekuja wakati Baraza la Usalama limedhirihisha kutoweza kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, kutokana na nguvu za kura ya turufu ya Moscow.

Kwa mtizamo wa Marekani, ni wazi kuwa Urusi imetumia vibaya haki yake ya kura ya turufu kwa miongo miwili na rasimu inayopendekezwa inalenga kurekebisha hilo.

Wenaweser anasema rasimu hiyo ina lengo la "kukuza jukumu la Umoja wa Mataifa, kukuza ushirikiano wa pande nyingi na kukuza sauti ya kila mmoja ambao sio wamiliki wa kura ya turufu na ambao hawako kwenye Baraza la Usalama kuhusu masuala ya amani na usalama wa kimataifa.

Bruce Amani/AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW