UN kutoa azimio jipya kuhusu Sahara Maghrabi
25 Aprili 2013Lakini azimio hilo halitakipa kikosi hicho haki za kufanya shughuli za uangalizi kama ilivyotakiwa na Marekani. Nchi ya Morocco ilianza kulikalia eneo la Sahara Magharibi ambalo ni koloni la zamani la Uhispania mwaka 1975, katika hatua ambayo haikukubaliwa na jumuiya ya kimataifa. Juhudi za Umoja wa Mataifa kutafuta amani kati ya Morocco na chama cha Polisario, kinachopigania uhuru wa eneo hilo zilikwama.
Mswada wa azimio la sasa, ambao shirika la habari al AFP lilifanikiwa kupata nakala yake, unaongeza muda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa katika eneo hilo, kinachojulikana kama MINURSO, hadi April 30, 2014. Azimio hilo pia lina lugha inayozihamasisha pande husika kuendelea na juhudi zao za kuendeleza na kulinda haki za binaadamu katika Sahara ya Magharibi na katika kambi za wakimbizi zilizoko Tindouf.
Jukumu la uangalizi wa haki za binaadamu
Marekani ilikuwa imependekeza kuwa na azimio linalotaka kikosi cha Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu la uangalizi na kuripoti kuhusu haki za binaadamu katika Sahara ya Magharibi na katika kambi za wakimbizi zinazoendeshwa na chama cha Polisario - hatua iliyopelekea kampeni ya hasira ya ushawishi kutoka kwa Morocco. Katika dalili ya wazi ya kuonyesha kutoridhishwa kwa utawala mjini Rabat, Morocco ilisimamishwa mazoezi ya kila mwaka ya kijeshi kati yake na Marekani, na kuanzisha kampeni ya ushawishi mjini Washington na ndani ya Uingereza, Uhispania, na Ufaransa, ambazo ni wanachama wa kundi la marafiki wa Sahara Magharibi, pamoja na Marekani na Urusi, kubadilisha azimio hilo.
Mwisho Marekani ililazimika kuachana na madai yake ya kujumlisha jukumu la uangalizi wa haki za binaadamu katika majukumu ya kikosi hicho, na mazoezi ya kivita yalirejelewa kwa kiwango kidogo. Kupewa jukumu la uangalizi wa haki za binaadamu kwa kikosi hicho ndilo jambo lililokuwa linapiganiwa sana na makundi ya haki za binaadamu na chama cha ukombozi wa Sahara Magharibi cha Polisario kwa miaka mingi, huku kukiwa na madai ya mateso dhidi ya wanaharakati wa Sahrawi, yanayofanywa na vikosi vya Morocco.
Kiokosi cha Umoja wa Mataifa katika Sahara ya Magharibi ndicho pekee duniani kote, kisicho na mamlaka ya kuangalia haki za binaadamu. Wataalmu wa Umoja wa Mataifa wanasema pia katika eneo hilo wamekuwa wakiteswa. Azimio jipya linatoa wito kwa pande zote kushirikiana na kikosi cha MINURSO, ikiwa ni pamoja na kuchanganyika kwa uhuru zaidi na washiriki wa mazungumzo.
Mvutano kati ya Morocco na Polisario
Azimio hilo pia linasisitiza kuungwa mkono kwa mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Christoper Ross, ambaye hakuaminiwa na Morocco kwa muda mwaka uliopita, ambaye amekamilisha ziara ya kanda iliyompeleka Ravab na El Auiun, mji mkubwa zaidi katika Sahara ya Magharibi.
Kwa miaka kadhaa, maazimio ya kurefusha mamlaka ya MINURSO yameibua mjadala kuhusu haki za binaadamu. Azimio la mwaka uliopita lilisema tu kwamba ilikuwa ni muhimu kuboresha hali ya haki za binaadamu katika Sahara ya Magharibi na kambi za wakimbizi za Tindouf.
Morocco ililiteka eneo la Sahara ya Magharibi katika miaka ya 1970, na inapendekeza eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini ya phosphate liwe na uhuru mpana chini ya himaya yake. Lakini hili linapingwa na chama cha Polisario, ambacho kinasisitiza juu ya haki ya Wasahara wenyewe kuamua katika kura ya maoni itakayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, iwapo wanataka uhuru au la.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Josephat Charo