UN: Maelfu ya raia wayakimbia mapigano Sudan
13 Januari 2025Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM) limeeleza jana Jumapili kuwa ndani ya muda wa siku tano tu, familia kutoka kwenye kaya 1,000 hadi 3,000 zimelazimika kuuhama mji wa Um Rawaba katika jimbo la Kordofan Kaskazini linalopatikana kusini mwa Sudan.
Wiki iliyopita, mapigano yalizuka katika eneo hilo kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, wakati jeshi lilipokuwa likiendesha operesheni ya kusonga mbele katika jimbo la Al-Jazira, takriban kilomita 300 kaskazini mashariki mwa Sudan.
Soma pia: Umoja wa Mataifa wasema zaidi ya wasudan milioni 30 wanahitaji msaada.
Wananchi wamekuwa wakishangilia baada ya jeshi kuukomboa mji wa Wad Madani kutoka mikoni mwa vikosi vya RSF. Elweya Hussein ni mmoja wao:
"Tuliishi miaka ya uchungu, pamoja na makafiri. Asante Mungu, leo tunamshukuru Mungu. Tumetoka gizani kuelekea kwenye nuru."
Shirika la IOM limesema familia hizo zilikimbia kutokana na kuongezeka kwa wasiwasi wa usalama kufuatia kuendelea kwa mapigano katika eneo hilo. Kulingana na takwimu za hivi punde za Umoja wa Mataifa zilizotolewa Jumatano iliyopita, zaidi ya watu 205,000 wameyahama makazi yao kwa sasa katika jimbo la Kordofan Kaskazini.
Soma pia: Kiongozi wa wanamgambo wa Sudan asema amepoteza mji mkuu wa jimbo la Al-Jazira
Takriban Wasudan milioni 11.5 ni wakimbizi wa ndani huku wengine wapatao milioni 3 wakiihama nchi hiyo, katika kile ambacho Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.
Mapigano yaendelea kuripotiwa katika maeneo mengine
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limesema hapo jana kuwa mtu mmoja aliuawa katika kile ilichokitaja kama "shambulio la kuchukiza" kwenye moja ya gari zake za kuwabeba wagonjwa katika jimbo la Darfur.
Shirika hilo limesema kuwa siku ya Ijumaa, gari hiyo ya wagonjwa ilikuwa imembeba mwanamke aliyekuwa na uchungu wa kujifungua ambaye alihitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura kutoka kambi ya watu waliohamishwa ya Zamzam kuelekea Hospitali ya Saudi ya mji huo. Hii ni mara ya pili kwa gari la wagonjwa la MSF kushambuliwa kwa risasi huko El-Fasher katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.
Kwa miezi kadhaa sasa, El-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, umekuwa ukishuhudia mapigano makali, na ni mji pekee katika eneo kubwa la magharibi mwa Sudan ambalo wanamgambo wa RSF hawajafanikiwa kulidhibiti.
Soma pia: Marekani yaishutumu Urusi kwa kufadhili vita Sudan
MSF ni mojawapo ya mashirika machache ya kimataifa ambayo bado yanahudumu katika jiji hilo, huku karibu vituo vyote vya matibabu vikiwa vililazimika kufungwa kutokana na kushambuliwa mara kwa mara.
Vita vya Sudan vilianza Aprili mwaka 2023 kati ya jeshi la taifa likiongozwa na Abdel Fattah al-Burhan linalopambana na vikosi vya RSF chini ya kiongozi wao Mohamed Hamdan Daglo, vimegharimu maisha ya makumi kwa maelfu ya watu na kuitumbukiza nchi hiyo kwenye kitisho kikubwa cha njaa ambapo watu milioni 24.6, ikiwa ni karibu nusu ya jumla ya watu wa Sudan tayari wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula.
(Vyanzo: AFP, Reuters)