1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mamilioni ya watu waathiriwa na njaa kusini mwa Afrika

16 Oktoba 2024

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP limeonya kuwa mamilioni ya watu kote kusini mwa Afrika wanakabiliwa na njaa kwa sababu ya ukame wa kihistoria ambao unatishia kusababisha maafa makubwa ya kibinadamu.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP)
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP)Picha: Sascha Steinach/dpa/picture-alliance

Nchi tano ambazo ni Lesotho, Malawi, Namibia, Zambia, na Zimbabwe, zimetangaza hali ya janga la kitaifa katika muda wa miezi iliyopita kwasababu ukame huo umeharibu mazao na kuangamiza mifugo.

Katika taarifa, WFP imesema kuwa Angola na Msumbiji pia zimeathirika pakubwa na kuonya kuwa mgogoro huo unatarajiwa kuongezeka hadi kipindi kijacho cha mavuno mnamo Machi au Aprili mwaka ujao.

Takriban watoto milioni 21 wana utapiamlo

Msemaji wa WFP katika eneo la kusini mwa Afrika Tomson Phiri, amesema ukame wa kihistoria, umeathiri zaidi ya watu milioni 27 kote katika eneo hilo na kwamba takriban watoto milioni 21 wana utapiamlo.

Phiri amesemaWFPinasambaza chakula na kusaidia mipango ya misaada lakini imepokea karibu moja ya tano tu ya dola milioni 369 inazohitaji.