UN: Mauaji ya Khashoggi ni mauaji yalio kinyume cha sheria
26 Oktoba 2018Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa Agnes Callamard, amesema Saudi Arabia yenyewe ilikubali kuwa mauaji hayo yalipangwa na kuwahusisha baadghi ya maafisa wa taifa lake. Amesema hatua ya iwapo walitekeleza mauaji hayo kutokana na amri ya taifa hilo ni jambo linalopaswa kuchunguzwa.
Wiki iliopita rais wa Marekani Donald Trump alisema wauaji wa kujitegemea ndio wanaopaswa kulaumiwa katika mauaji hayo.
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir pia alinyoosha kidole cha lawama kwa operesheni ya kujitegemea kwa mauaji ya Jamal Khashoggi kabla ya ufalme huo kunukuu taarifa kutoka Uturuki kuwa mauaji hayo huenda yakawa yamepangwa.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema muendesha mashtaka wa Saudia anatarajiwa mjini Istanbul jumapili kukutana na mwenzake wa Uturuki ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa mauaji ya Jamal Khashoggi.
Urusi imesema inaamini Ufalme wa Saudia haukuhusika na mauaji hayo. Tamko hili limejiri baada ya rais wa Urusi Vladimir putin kuzungumza kwa njia ya simu juu ya kisa hicho na mwanamfalme Mohammed bin Salman.
Mwanae Khashoggi Salah Khashoggi ameondoka Saudi Arabia kuelekea Marekani
Khashoggi, muandishi wa gazeti la Washington post nchini Marekani mkosoaji mkubwa wa sera za mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman alikuwa uhamishoni nchini Marekani kwa takriban mwaka mmoja.
Aliuwawa tarehe 2 Oktoba katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia nchini Uturuki lakini hadi sasa mwili wake haujapatikana. Serikali ya Uturuki wamechapaisha maelezo yanayodai mwanahabari huyo aliteswa kuuwawa na viungo vyake kukatwa katwa.
Katika hotuba yake ya kwanza juu ya mauaji hayo Mwanamgfalme Mohammed bin Salman alisema amehuzunishwa na mauaji hayo na kwamba tayari maafisa 18 wa Saudi Arabia wametiwa nguvuni na wanahojiwa.
Wakati huo huo mtoto wa Jamal Khashoggi Salah Kahshoggi ameondoka Saudi Arabia na kuelekea Marekani baada ya ufalme huo kumuondolea marufuku ya kusafiri.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Robert Palladino amesema Marekani imekaribisha uamuzi wa Salah Kashoggi na familia yake kuingia nchini humo. Mahali atakapoishi hapajulikani hasaa lakini baabake alikuwa akiishi mjini Washington.
Mwandishi Amina Abubakar/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman