UN: Mauaji ya kimbari bado yanaendelea Myanmar
25 Oktoba 2018Akiwasilisha ripoti jana katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Darusman amesema mbali na mauaji ya watu wengi, mzozo huo una lengo la kuwaangamiza kabisa Warohingya, kuzuia uzazi pamoja na kuwatawanya katika makambi mbalimbali.
Ripoti hiyo yenye kurasa 444 ambayo ilitangazwa hadharani kwa mara ya kwanza mwezi uliopita, imelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kulipeleka suala la Myanmar katika Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa, ICC, The Hague au kuanzisha mahakama mpya ya uhalifu wa kivita kama ilivyofanya kwa iliyokuwa Yugoslavia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maafisa wa ngazi ya juu wa kijeshi, akiwemo mkuu wa majeshi, Min Aung Hlaing lazima wachunguzwe na kushtakiwa kwa mauaji ya kimbari katika jimbo ya Rakhine.
Darusman amesema maelfu ya Warohingya bado wanakimbilia Bangladesh na kiasi ya watu 250,000 hadi 400,000 ambao wamebaki wanaendelea kukumbana na mateso pamoja na ukandamizaji.
''Bila uwajibikaji, hapawezi kuwa na utaratibu endelevu kwa Warohingya kurejea salama Myanmar. Warohingya watarejea vipi nyumbani, ambako mateso bado yanaendelea na wahalifu wanaendelea kulindwa? Kweli tunatarajia warejee kwa kuviamini tena na kutegemea ulinzi wa vikosi vya usalama ambavyo viliwaua, kuwabaka na kuziharibu jamii zao?'' aliuliza Darusman.
Myanmar yakanusha madai
Hata hivyo, Myanmar imekuwa ikikanusha madai kwamba jeshi lake linafanya unyama huo na imedai kuwa ghasia nchini humo zilisababishwa na wapiganaji wa Rohingya ambao walivishambulia vituo vya kijeshi katika eneo la mpaka Agosti mwaka uliopita wa 2017.
Balozi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa, Hau Do Suan ameiita ripoti hiyo '' yenye lengo la kuichafua Myanmar na iliyochochewa kisiasa'' na amesema serikali ya nchi yake inayakataa madai ya kuwepo mauaji ya kimbari.
Aidha, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar, Christine Schraner Burgener amesema uwajibikaji ni mojawapo ya nguzo mbili muhimu za upatanisho wa kitaifa, na nyingine ni majadiliano ya pamoja.
Hata hivyo, uwasilishaji wa ripoti hiyo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ulipitishwa kwa kura ya ''ndiyo'' na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uholanzi, Sweden, Cote d'Ivoire, Kuwait, Peru na Poland. China, mshirika wa karibu wa Myanmar pamoja na Urusi na Bolivia zilipiga kura ya ''hapana'', huku Equatorial Guinea, Ethiopia na Kazakhstan zikijizuia kupiga kura.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba