1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSudan

UN: Msaada wa chakula Sudan wakaribia kuisha

16 Januari 2026

Umoja wa Mataifa umesema kuwa msaada wa chakula unatarajiwa kuisha nchini Sudan ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi.

Sudan, Bandari ya Sudan 2025 | Msaada wa chakula wa WFP kwa Khartoum ukipakiwa kwenye malori
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaelezea hofu ya Sudan kukumbwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu kufuatia uhaba wa misaada ya chakula.Picha: The Yomiuri Shimbun/AP Photo/picture alliance

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu kumalizika kwa misaada ya chakula, hali inayozusha hofu kwa mamilioni ya watu walioko katika mzozo mkubwa zaidi wa njaa duniani, na huku mazungumzo ya amani yakionyesha maendeleo madogo.

Ross Smith Mkurugenzi wa Uratibu wa Kukabiliana na Mahitaji ya Dharura wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, amesema kuwa akiba yao ya chakula nchini Sudan itakuwa imepungua ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi. Smith amesema bila ya kupata ufadhili wa ziada wa haraka, mamilioni ya watu wataachwa bila msaada muhimu wa chakula ndani ya wiki chache zijazo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 21, ambao ni takribani nusu ya idadi ya watu wa Sudan, sasa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku theluthi mbili ya idadi ya watu wakihitaji msaada wa dharura.

Aidha, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, anayeizuru Sudan amesema watu wengi walioyakimbia makaazi yao hawana makaazi ya kutosha, huku wanawake wakiwa na uwezo mdogo wa kuzifikia huduma muhimu za misaada. Türk aliyeko Dongola, mji mkuu wa Jimbo la Kaskazini mwa Sudan, ametoa wito wa juhudi zote muhimu kufanywa na mamlaka za Sudan na jumuia ya kimataifa ili kuwezesha utoaji wa misaada muhimu.

Türk amekutana na zaidi ya wawakilishi 50 kuzungumzia ''changamoto zinazowakabili watu wa Sudan na mahitaji muhimu ya watu waliohamishwa kutokana na vurugu kubwa katika maeneo ya Darfur na Kordofan. Amesema watu hao wamezungumzia kuhusu madhila na hali mbaya inayowakumba watu wa maeneo hayo.

''Hawana makaazi ya kutosha kwa wale waliozikimbia nyumba zao ndani ya nchi. Hakuna suluhisho la kueleweka kwa wanawake ambao wameathiriwa na unyanyasahi wa kingono. Hakuna umakini wa kutosha unaotolewa kwa watu wanaoishi na ulemavu. Lakini wawakilishi hawa pia wamepata suluhisho. Kuna haja  ya kuwa na juhudi kubwa, ndani ya Sudan na jumuia ya kimataifa, kuwasaidia kurahisisha kazi yao ili waweze kutoa msaada wa kibinaadamu unaohitajika sana kulingana na mazingira yaliyopo,'' amesema Türk.

Wito watolewa kwa jumuiya ya kimataifa kufadhili misaada kwa SudanPicha: UNICEF/Xinhua/picture alliance

UNICEF: Mamilioni ya watoto wako katika hatari kubwa

Wiki iliyopita, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF lilisema kuwa mamilioni ya watoto hawana msaada na wako katika hatari kubwa, na kwamba misaada ya kiutu bado ''haitoshi'', huku kukiwa na uhaba wa fedha na mapigano yanayoendelea.

Mwezi Desemba, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR lilisema kuwa wimbi la kupunguzwa misaada na ''kutowajibika kwa kiasi kikubwa'' kulisababisha mateso yasiyo ya lazima kwa watu wenye uhitaji.

Smith amesema WFP imelazimika kupunguza mgao hadi "kiwango cha chini kabisa cha kuishi" na ameonya kwamba faida zilizopatikana kwa shida za awali katika maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa zina hatari ya kubadilishwa. WFP imesema inahitaji dola milioni 700 za dharura ili kuendelea na shughuli zake hadi mwezi Juni.

Siku ya Jumatano, mshauri wa ngazi ya juu wa Marekani kuhusu masuala ya Uarabuni na Afrika, Massad Boulos alisema Umoja wa Mataifa uliwasilisha zaidi ya tani 1.3 za mahitaji ya kibinaadamu huko El-Fasher, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mji huo ulipozingirwa mwezi Mei, mwaka 2024.

Kulingana na IRC, Sudan bado yaongoza mataifa yenye mizozo duniani.

AFP, AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW