1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mzozo wa Israel na Hamas umefikia hatua mbaya

Angela Mdungu
16 Oktoba 2023

Umoja wa Mataifa umesema mzozo kati ya Israel na Hamas umefikia hatua mbaya wakati hospitali za Gaza zikikaribia kuishiwa akiba ya nishati na juhudi za kupitisha misaada ya kiutu katika mpaka wa Rafah zikiendelea.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: Sergei Bobylev/ITAR-TASS/IMAGO

Umoja wa Mataifa kupitia Katibu Mkuu Antonio Guterres umetoa wito kwa kundi la Hamas liwaachilie huru mateka huku ukiitaka Israel kuruhusu misaada ifike katika Ukanda wa Gaza. Guterres amesema Umoja huo una chakula, maji, dawa na mafuta ambayo tayari yako Misri na katika ukingo wa magharibi kwa ajili ya kupelekwa Gaza kama wafanyakazi wake wataruhusiwa kuvisafirisha bila ya vikwazo.

Guterres ametoa kauli hiyo wakati ambapo zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao huku Israel ikitarajiwa kufanya uvamizi unaolenga kuliangamiza kundi la Hamas, lililovamia kusini mwa Israel zaidi ya wiki moja iliyopita.

Soma zaidi: UN: Takriban watu milioni moja watoroka makazi yao Gaza

Wito wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa umetolewa wakati mashirika ya misaada ya kiutu yakifanya juhudi za kuingiza misaada Gaza katika mzozo ambao umesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 2,600.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imevinukuu vyombo vya habari vya Misri vilivyoripoti kuwa huenda mpaka waRafah kuingia Gaza ukafunguliwa kwa muda leo Jumatatu.

Wakaazi wa Gaza baada ya mashambulizi ya anga ya IsraelPicha: Belal Khaled/Anadolu/picture alliance

Awali shirika la habari la Reuters liliripoti likivinukuu vyanzo vya kiusalama vya Misri ambavyo halikuvitaja vikidai kuwa kungekuwa na usitishaji mapigano kuanzia saa tatu asubuhi suala ambalo pande zote mbili za mzozo zimekanusha.

Taarifa ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema kuwa kwa sasa hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa na misaada katika ukanda wa Gaza iliyopitishwa ili kuwatoa raia wa kigeni nje ya eneo hilo.

Israel yawahamisha raia wake mpakani na Lebanon

Wakati hayo yanajiri, jeshi la Israeli limesema kuwa linawahamisha wakazi wa maeneo yaliyo karibu na mpaka wake na Lebanon, kaskazini mwa Israel. Wanaohamishwa ni wakaazi katika vijiji 28 vilivyo umbali wa kilometa 2 kutoka katika mpaka huo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mashambulizi yaliyofanywa kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon na kusababisha kifo cha mtu mmoja. 

Wanajeshi wa Israel wakiwa karibu na mpaka wa Israel na LebanonPicha: ARIS MESSINIS/AFP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Antony Blinken amerejea Israel leo baada ya kufanya mazungumzo na maataifa sita ya kiarabu, kwa matumaini ya kuratibu juhudi dhidi ya kundi la Hamas. Blinken amefanya pia ziara hiyo akitafuta namna ya kuutatua mzozo wa Kiutu unaoikabili Gaza.

Amerejea Israel akitarajiwa kukutana na viongozi wa nchi hiyo wakati ikijiandaa kuanza operesheni kubwa ya ardhini dhidi ya kundi la Hamas katika mji wa Gaza.

Hamas inazingatiwa na Marekani, Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani na baadhi ya mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW