1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN na tume ya haki za binadamu Ethiopia zataka raia walindwe

4 Julai 2021

Tume ya kutetea haki za binadamu ya Ethiopia (EHRC), imetilia mkazo miito ya Umoja wa Mataifa kutaka hatua za dharura zichukuliwe kuwalinda na kuwasaidia raia katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Äthiopien | Jubel beim Einmarsch der TDF in Mekelle
Picha: DW

Jimbo hilo limekumbwa na uharibifu wa miundo mbinu muhimu huku kitisho cha njaa kikiongezeka kufuatia machafuko ambayo yamedumu kwa miezi minane sasa.

Mamilioni ya watu wanakabiliwa na kitisho cha njaa mnamo wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vikifikia hatua ya mabadiliko na maelfu ya wanajeshi wa Ethiopia waliokamatwa wakiwasili katika mji mkuu wa jimbo la Tigray Mekele, huku waasi wakitangaza kurejesha udhibiti wa mji huo mikononi mwao.

Jimbo la Tigray limekuwa eneo la mapigano tangu Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipopeleka jeshi mapema mwezi Novemba kupindua utawala ulioasi wa jimbo hilo, wa Chama cha Ukombozi wa Tigray (Tigray People's Liberation Front-TPLF).

Abiy ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2019, aliwatuhumu waasi kufanya mashambulizi dhidi ya kambi za jeshi la Ethiopia.

Waasi wapuuza tangazo la usitishwaji vita

Baada ya mafanikio ya mapema na hata kutangaza ushindi, vikosi vya serikali ya shirikisho walikumbana na mapambano makali ya miezi kadhaa dhidi ya wapiganaji wa TPLF ambao kwa sasa walibadilisha jina kuitwa Vikosi vya Ulinzi vya Tigray (TDF).

Vikosi vya Ethiopia vilisaidiwa na vikosi vya jimbo jirani la Amhara pamoja na jeshi la taifa jirani Eritrea.

Mnamo Jumatatu, TDF ilirudisha mji wa Mekele mikononi mwake baada ya kukamatwa na jeshi la Ethiopia tangu Novemba 28.

Wapiganaji wa TDF wametangaza kurejesha udhibiti wa mji wa Mekele mikononi mwaoPicha: DW

Serikali ya Ethiopia mjini Addis Ababa kwa haraka ilitoa tangazo la pamoja la usitishwaji vita. Lakini waasi walilitizama tangazo hilo kama mzaha, badala yake walipuuza na kuapa kuendelea mbele kupigana.

Mnamo siku ya Ijumaa, idadi kubwa ya wanajeshi wa Ethiopia ambao ni wafungwa waliwasili Mekele kwa miguu na wengine kwa malori. Mwandishi mmoja wa habari wa shirika la habari la AFP aliripoti hayo.

Kulingana na TDF, zaidi ya wanajeshi 7,000 wa Ethiopia walitembea kilomita 75 (maili 50) kwa siku nne kutoka mji wa kusini magharibi Abdi Eshir kuingia Mekele.    

Viongozi wa TPLF warudi Mekele     

Viongozi wa utawala wa zamani wa jimbo hilo akiwemo mwenyekiti Debretsion Gebremichel wamerudi Mekele baada ya miezi kadhaa ya kusakwa na jeshi la Ethiopia.

TDF sasa inatarajiwa kuelekeza nguvu zao kuelekea pande za magharibi na kusini mwa jimbo hilo, ambayo yalikamatwa na kuchukuliwa na vikosi vya Amhara mwanzoni mwa machafuko hayo.

Waamhara wanaamini TPLF walichukua maeneo hayo katika miaka ya 1990 kinyume cha sheria na kuyafanya maeneo yao.

Mnamo Ijumaa, Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yalitoa tahadhari kufuatia kuharibiwa kwa madaraja mawili muhimu kuingia Tigray.

Uharibifu wa miundombinu wazusha wasiwasi

Watetezi wa haki za binadamu washutumu uharibifu dhidi ya miundombinu muhimu kuingia TigrayPicha: Roger Sandberg/AP/picture alliance

Kulingana na Umoja wa Mataifa, daraja muhimu liliripotiwa kuharibiwana vikosi vya Amhara, lakini serikali ya Ethiopia ilivinyooshea vidole vya lawama vikosi vya Tigray.

Serikali ya shirikisho ilituhumiwa kuhusika na uharibifu huo mkama hatua ya kuzuia misaada ya kiutu isifikishwe Tigray. Hata hivyo imekana madai hayo.

"Usalama wa raia ni sharti usalie kuwa kipaumbele. Hivyo ni sharti hatua za dharura zichukuliwe,” imesema tume ya Haki za binadamu ya Ethiopia EHRC.

Tume hiyo imesema ina wasiwasi kuhusu kukatizwa kwa umeme, huduma za mawasiliano Pamoja na za maji katika maeneo kadhaa ya jimbo hilo, hatua zinazofanya hali ya maisha kuwa ngumu.

"Uharibifu dhidi ya miundo mbinu za rai ani jambo lisilokubalika abadan, ni muhimu kuwe na usitishwaji kamili wa vita ili kusafisha njia kwa mazungumzo yatakayoleta suluhisho la kisiasa” alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Jumamosi.     

Watu 400,000 wakabiliwa na kitisho cha njaa Ethiopia

Mnamo siku ya Ijumaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha kwanza cha wazi kuhusu mzozo wa Tigray.

Ramesh Rajasingham, kaimu mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa. Picha: UNOCHA/Naomi Frerotte

Ramesh Rajasingham ambaye ni kaimu mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa alikiambia kikao hicho kwamba hali "imezidi kuwa mbaya” tangu kurejea tena kwa makabiliano baina ya pande hasimu wiki za hivi karibuni.

"Zaidi ya watu 400,000 wanakadiriwa kuwa kwenye kundi la wanaoukumbwa na baa la njaa na wengine milioni 1.8 wanakaribia kukumbwa na ukosefu wa chakula,” amesema Rajasingham.

Rajasingham ameongeza kuwa mashirika mengine yanakadiria kuwa idadi ni kubwa kuliko inayotajwa na kwamba zaidi ya watoto 33,000 wana utapiamlo mkali.

Tume ya EHRC imetoa wito kwa pande zote kusitisha vita ili kuwezesha ugavi wa misaada ya kiutu na vilevile kuwezesha wakulima kurejea katika mashamba yao kufanya kilimo.

(AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW