1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN: Ni hatari kusitisha ufadhili kwa shirika la UNRWA

31 Januari 2024

Wakuu wa mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa wameonya kwamba kusitisha ufadhili kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, kutakuwa na "matokeo mabaya" kabisa kwa Ukanda wa Gaza.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA Philippe Lazzarini (kushoto).
Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Kamati ya Kudumu ya Mashirika ya Kimataifa imetoa tamko la pamoja na kuonya kwamba kusitisha fedha za ufadhili kwa shirika hilo la UNRWA ni hatari na kunaweza kusababisha kuporomoka kwa mfumo wa kibinadamu na kutokea athari kubwa ya kibinadamu huko Gaza. Hatua hiyo inaweza pia kusababisha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu na hata kata katika ukanda mzima.

Soma pia: WHO yalaani shambulio la Israel dhidi ya hospitali Gaza

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mfanyakazi yeyote wa Umoja wa Mataifa anayehusika na vitendo vya ugaidi atawajibishwa kama alivyosema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, huku ikisisitiza kuwa hawapaswi kuzuia shirika zima kutekeleza wajibu wake wa kuwahudumia watu wenye uhitaji mkubwa.

Wapalestina wakijaribu kuzima moto katika jengo la kituo cha mafunzo ya ufundi cha UNRWA ambacho watu waliokimbia makazi yao wanakitumia kama makazi ya muda, baada ya kulengwa na mashambulizi ya Israel huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza: 24.01.2024.Picha: Ramez Habboub/AP Photo/picture alliance

Baadhi ya mataifa ambayo ni wafadhili wakuu wa UNRWA, yakiwemo Marekani, Ujerumani na Japan, yalitangaza kusitisha ufadhili wao kwa shirika hilo kufuatia madai ya Israel kwamba baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA   walihusika katika mashambulizi ya kigaidi ya Hamas ya Oktoba 7.

UNRWA ilisema ilichukua hatua kuhusu madai hayo ya Israel, kwa kuwafuta kazi mara moja wafanyakazi wake kadhaa wanaotuhumiwa na kwamba wameanzisha uchunguzi wa kina.

Soma pia: UN: Hali katika hospitali za Gaza ni mbaya mno

Taarifa hiyo ya pamoja imeyahimiza mataifa wafadhili kutafakari upya hatua yao ya kusitisha ufadhili huo, ikisisitiza kwamba hakuna shirika lingine lolote lenye uwezo na vifaa vya kuipatia Gaza kiwango cha misaada ambacho kinatolewa na shirika la UNRWA lenye jumla ya wafanyakazi wapatao 13,000 na likiwa ndilo shirika muhimu la kibinadamu huko Gaza.

Mapigano yaendelea kuripotiwa Gaza

Wapalestina waliojeruhiwa wakati wa mashambulizi ya anga na ardhini ya Israel huko Khan Younis wakifikishwa hospitalini huko Rafah katika Ukanda wa Gaza: 23.01.2024.Picha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema kuwa vikosi vya Israel vimevamia Hospitali ya Al-Amal iliyoko katika mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis, ambako ni kimbilio la takriban watu 7,000 waliolazimika kuyahama makaazi yao. Madaktari katika  hospitali za Khan Younis wanafanya kazi katika mazingira magumu. Daktari Karam Madboul, ni kutoka hospitali ya Nasser Medical Complex:

"Kwa sasa, tunafanya kazi katika mazingira ambayo yasiyofaa kwa huduma ya afya. Ni mazingira ambayo yanaruhusu kuenea kwa maambukizi kati ya wagonjwa. Hakika, kuna uhaba mkubwa wa vifaa, dawa na wahudumu wa afya."

​Wakati huo huo, wanajeshi wa Israel waliovalia mavazi ya kike walivamia hospitali ya Ibn Sina kaskazini mwa mji wa Jenin  katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuwaua Wapalestina watatu inaodai ni wanaharakati wa makundi ya wapiganaji.

Aidha, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekataa matakwa ya Hamas wakati wa mazungumzo yasiyo rasmi ya kutaka usitishwaji mapigano, akisema Israel haitawaondoa maelfu ya wanajeshi wake huko Gaza wala kuwaachilia wanaharakati wa Hamas walio kifungoni.

Hospitali katika Ukanda wa Gaza zaelemewa

02:03

This browser does not support the video element.

(ap,dw)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW