UN yasema watu 100 wameuawa Libya tangu Aprili
30 Julai 2020Ujumbe wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, umesema kwenye ripoti yake kuwa zaidi ya raia 250, walijeruhiwa katika kipindi hicho. Hiyo ilikuwa ni ongezeko la asilimia 276 ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa waathiriwa wakuu ni wakaazi wa magharibi mwa Libya, ambayo imekuwa kitovu cha mapigano kati ya vikosi vya mashariki vinavyoongozwa na kamanda Khalifa Haftar pamoja na wanamgambo kadhaa ambao ni washirika wao dhidi ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya mjini Tripoli.
Chanzo cha machafuko ya Libya
Libya ilitumbukia kwenye machafuko wakati vuguvugu la mwaka 2011 lililoungwa mkono na Jumuia ya Kujihami ya NATO, lilipomuondoa madarakani aliyekuwa rais Muammar Gaddafi, ambaye baadaye aliuawa.
Taarifa zaidi: Libya: Pande hasimu kuanza tena mazungumzo
Nchi hiyo kwa sasa imegawika mara mbili kati ya vikosi pinzani vinavyodhibiti mashariki mwa taifa hilo, na vikosi vya serikali inayotambuliwa kimataifa vinavyodhibiti magharibi. Kila upande ukiungwa mkono na makundi yenye silaha na serikali tofauti za nje.
Mnamo Aprili 2019, vikosi vya Haftar vilianzisha mashambulizi ya kutaka kuchukua udhibiti wa mji mkuu Tripoli. Lakini kampeni ya Haftar ilishindwa mwezi uliopita wakati vikosi vya Tripoli pamoja na wanamgambo washirika wao na kwa usaidizi wa Uturuki, viliulemea upande wa Haftar viungani mwa mji wa Tripoli na katika miji mingine magharibi mwa nchi hiyo. Haftar anaungwa mkono na Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi.
Nchi za nje katika vita vya Libya
Vikosi vya Tripoli vinaungwa mkono na Uturuki ambayo ni adui mkubwa wa Misri pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusiana na mzozo mpana wa kikanda na siasa za kidini ya Uislamu, pia kwa usaidizi wa Qatar ambalo ni taifa tajiri la Ghuba.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umesema ulirekodi miili 85 ya raia pamoja na zaidi ya watu 230 waliojeruhiwa magharibi mwa Libya. Umeongeza kwamba watu wasiopungua 22 waliuawa na zaidi ya kumi kujeruhiwa eneo la kati nchini Libya, lakini ni watu wawili pekee walijeruhiwa upande wa mashariki mwa nchi hiyo ambao una utajiri mkubwa wa mafuta.
Taarifa zaidi: Umoja wa Mataifa wafichua njama za kijeshi nchini Libya
Ripoti hiyo imesema vikosi vya Haftar ndivyo vilihusika kwa asilimia 80 ya maafa, au viliwaua watu 75 na kuwajeruhi watu 212.
Imeendelea kusema kuwa vikosi vya Tripoli na washirika wake viliwaua takriban watu 30, na kuwajeruhi takriban wengine 50. Idadi iliyosalia ya waliouawa haikujulikana waliuawa na vikosi vipi.
Vifo vingi vilitokana na mashambulizi ya ardhini
Kulingana na ripoti hiyo, mashambulizi ya ardhini yalisababisha vifo vya raia 69 na kuwajeruhi watu 195, huku wengine zaidi ya 20 waliuawa na 14 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya angani.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulisema raia 17 waliouawa miongoni mwao wanawake na watoto wanne walishambuliwa na ndege isiyohitaji rubani ya Uturuki yaani drone mnamo Juni 3, wakati wa shambulizi lililofanywa katika mji wa Oasr Bin Ghashir magharibi mwa Libya, kusini mwa Tripoli. Raia wengine 14 pia walijeruhiwa kwenye shambulizi hilo.
Ripoti hiyo pia imerekodi mashambulizi tisa dhidi ya shule, tisa dhidi ya vituo vya afya na moja dhidi ya gari la wagonjwa mnamo robo ya pili ya mwaka. Ujumbe huo umevilaumu vikosi vya Haftar kwa mashambulizi saba kati ya hayo yote.
Hospitali ya Khadra iliyoko Tripoli iliyopaswa kuwatibu wagonjwa wa COVID-19, ilishambuliwa mara nne tofauti kwa roketi.
Siku mbili baada ya kuzungumza na maafisa wa serikali inayotambuliwa kimataifa ya Libya, mwanadiplomasia wa Marekani nchini Libya Joshua Harris, alikutana na wabunge wa mashariki mwa Libya, pamoja na maafisa wa kijeshi mjini Benghazi. Ikiwa ni katika juhudi zake za kujaribu kuzuia mapigano ya kuchukua udhibiti wa mji wa bandari wa Sirte ambao ni wa kimkakati.
Aidha Harris juhudi za Harris ni kuiwezesha kampuni ya taifa ya mafuta Libya kuanza tena kusafirisha mafuta, baada ya shughulizake kufungwa na vikosi vya Haftar.
Mwandishi: John Juma
Mhariri: Iddi Ssessanga