1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

UN: Raia 18,000 wauawa au kujeruhiwa Ukraine

28 Desemba 2022

Umoja wa Mataifa umesema idadi ya raia waliouawa au kujeruhiwa katika vita vya Ukraine imefikia takribani 18,000, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine miezi 10 sasa.

Ukraine-Krieg - Cherson
Picha: Kherson Region Administration/AP/dpa/picture alliance

Taarifa iliyotolewa Jumanne usiku na Ofisi ya Kamnisha Mkuu wa Umoja wa Mataifa inayosimamia haki za binaadamu OHCHR, imeeleza kuwa idadi kamili ya raia wa Ukraine waliouawa huenda ikawa ya juu zaidi, lakini upatikanaji wa takwimu kutoka kwenye maeneo ya mapambano ni mgumu.

Watoto 429 wameuawa

Kwa mujibu wa OHCHR, kuanzia Februari 24 wakati Urusi ilipoivamia Ukraine hadi Desemba 26, raia 6,884 wameuawa na raia 10,947 wamejeruhiwa. Miongoni mwa waliouawa ni watoto 429. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vifo vingi vilisababishwa na miripuko ya mabomu, makombora, mifumo ya kurushia roketi na mashambulizi ya anga.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema raia wengi wameuawa na kujeruhiwa katika jimbo la Donbass, ambako kuna mikoa ya Donetsk na Luhansk. Awali, Umoja wa Mataifa ulisema vikosi vya Urusi viliyashambulia kwa makombora maeneo yenye watu wengi na kuwaua raia na kuharibu hospitali, shule na miundombinu mingine ya kiraia. Katika siku za hivi karibuni Urusi imekuwa ikishambulia miundombinu ya nishati na maji.

Askari wa zimamoto akizima moto katika jengo lililoshambuliwa na makombora ya Urusi kwenye mji wa Kherson, UkrainePicha: Dimitar Dilkoff/AFP

Katika uwanja wa mapambano vikosi vya Urusi vimefyatua makombora 33 yakiyalenga maeneo ya raia kwenye mji wa Kherson katika muda wa saa 24 zilizopita hadi mapema Jumatano asubuhi. Mkuu wa Majeshi wa Ukraine, amesema leo kuwa makombora hayo yamerushwa Kherson, mji ambao ulikombolewa mwezi uliopita.

Mchambuzi wa jeshi la Ukraine, Oleh Zhdanov amesema mapigano yamepamba moto, huku Urusi ikipeleka vifaru zaidi na magari ya kivita katika maeneo ya mapambano. ''Mapigano yameongezeka katika mji wa Bakhmut na Avdivka, eneo ambalo linaunganisha mkoa wa Donetsk. Mapambano yameongezeka baada ya kupungua kwa siku kadhaa zilizopita,'' alifafanua Zhdanov.

Svatove na Kremina pia yashambuliwa

Nalo jeshi la Uingereza limesema kuelekea upande wa mashariki, mji wa Bakhmut umeshambuliwa vikali, huku mapigano yakiendelea pia kwenye miji ya kaskazini ya Svatove na Kremina.

Wakati huo huo, waziri wa serikali wa Ukraine anayehusika na masuala ya teknolojia, Mykhailo Fedorov amesema nchi hiyo imenunua baadhi ya ndege 1,400 zisizo na rubani, nyingi zikiwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi na inapanga kutengeneza mifumo ambayo inaweza kuzuia ndege zisizo na rubani za Urusi ambazo ilizitumia wakati ikiivamia Ukraine.

Waziri wa serikali wa Ukraine anayehusika na masuala ya teknolojia, Mykhailo Fedorov Picha: Yevhen Liubimov/Avalon/picture alliance

Katika mahojiano yake na shirika la habari la AP, Fedorov amevielezea vita vya Urusi nchini Ukraine kama vita kuu ya kwanza katika wakati huu wa matumizi ya mtandao wa intaneti.

Aidha, Sergei Kiriyenko mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Rais wa Urusi, Vladmir Putin amekitembelea kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia, kwa lengo la kuangalia usalama wa kinu hicho.

Italia na hofu ya kuipatia Ukraine mifumo ya kujikinga na makombora

Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Ulinzi wa Italia, Guido Crosetto ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuipatia Ukraine mifumo ya kujilinda na makombora, kama ambavyo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameomba.

Crosetto ameliambia Jumatano gazeti la Messagero, kwamba mifumo hiyo inaweza kutolewa iwapo itawezekana, lakini iwapo Italia itaipatia Ukraine mifumo ya kujilinda na makombora, wanapaswa kuzichukua kutoka kwenye akiba yao na inabidi kufanya hivyo bila kuzipunguza na kuwa na uhakika kuhusu ubora wake.

(AP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW