UN: Rwanda inao udhibiti na mamlaka kwa M23
2 Julai 2025
Ripoti hiyo iliyofichuliwa na shirika la habari la Reuters inaelezea msaada wa kijeshi ambao Rwanda iliutoa kwa wapiganaji wa M23 ikiwa ni pamoja na mafunzo na vifaa vya kiteknolojia vya hali ya juu vilivyokuwa na uwezo wa kuvuruga mifumo ya ulinzi wa anga wa jeshi la Kongo lililokuwa limeelemewa, jambo ambalo liliwapiga jeki waasi hao.
Wataalam hao wanasema hatua hiyo iliiwezesha Rwanda kuwa na ushawishi wa kisiasa na kuweza kulifikia eneo la mashariki mwa DRC lenye utajiri wa madini na lililokumbwa na mizozo kwa zaidi ya miongo mitatu.
Aidha ripoti hiyo imeendelea kubainisha kuwa Rwanda iliwapokea viongozi wa muungano wa waasi unaojumuisha M23 katika vituo vyake vya Gabiro, Nasho na Gako ambako wapiganaji wa M23 walipewa mafunzo ya kijeshi. Pia, wataalam hao wanasema Rwanda iliongeza idadi ya wanajeshi wake hadi kufikia 6,000 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini.
Wanadiplomasia wameeleza kuwa ripoti hiyo inayotarajiwa kuchapishwa hivi karibuni, iliwasilishwa mapema mwezi Mei kwa kamati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inayofuatilia mzozo wa Kongo na inayo husika pia na kuweka vikwazo.
Mwezi Januari na Februari, waasi wa M23 walipata mafanikio makubwa mashariki mwa Kongo kwa kuchukua udhibiti wa miji mikubwa zaidi eneo hilo ya Goma na Bukavu.
Rwanda yatajwa kuhusika moja kwa moja
Kwa muda kadhaa sasa, Kongo, Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi wamekuwa wakieleza bayana kwamba Rwanda inaiunga mkono M23 kwa kuipatia askari na hata silaha.
Hata hivyo serikali mjini Kigali imekuwa ikikanusha tuhuma hizo ikidai kuwa vikosi vyake vimekuwa vikijilinda dhidi ya jeshi la Kongo na wanamgambo wa kihutu wa FDLR ambao wanaohusishwa na mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi ya mwaka 1994 huko Rwanda.
Lakini ripoti hii iliyotolewa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa inakanusha madai hayo na kusema kuwa msaada wa jeshi la Rwanda kwa M23 haukulenga kimsingi kushughulikia vitisho vinavyotolewa na FDLR, na kwamba Kigali ililenga "kujinyakulia maeneo zaidi" huko mashariki mwa Kongo.
Mpaka sasa, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda na hata wasemaji wa serikali za Kongo na Rwanda hawajazungumza chochote juu ya ripoti hiyo. Ikumbukwe kuwa mnamo Juni 27, chini ya upatanishi wa Marekani, Rwanda na Kongo zilisaini makubaliano ya amani mjini Washington.
Mkataba huo hata hivyo umekosolewa na baadhi ya watu wakiutaja kama makubaliano ya kibiashara yatakayozinufaisha nchi za Magharibi kwa mabilioni ya dola hasa kutokana na uwekezaji wao katika eneo hilo tajiri lenye madini mbalimbali ikiwa ni pamoja na tantalum, dhahabu, cobalt, shaba na lithium. Lakini viongozi wa Kinshasa wanadai kuwa watalinda maslahi ya nchi yao.
(Chanzo: Reuters)