1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

UN: Syria inahitaji misaada ya kibinadamu

Babu Abdalla11 Machi 2021

Michelle Bachelet amezitolea mwito nchi kupitia mahakama zao za kitaifa kuendelea na kesi dhidi ya watuhumiwa wa visa vya uhalifu wa kivita nchini Syria.

Michelle Bachelet | UN Hochkommissarin für Menschenrechte
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na haki za binadamu Michelle BacheletPicha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayousika na haki za binadamu, Michelle Bachelet amezitolea mwito nchi kupitia mahakama zao za kitaifa kuendelea na kesi dhidi ya watuhumiwa wa visa vya uhalifu wa kivita nchini Syria wakati nchi hiyo inapoelekea kuadhimisha miaka 10 tangu kuzuka kwa vita nchini humo. 

Bachelet amesema jaribio la kuwasilisha kesi ya makosa ya uhalifu wa kivita yaliyofanyika nchini Syria katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC limefeli.

Ni mtu mmoja tu ndiye aliyehukumiwa katika mahakama ya kigeni kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu au kwa uhalifu wa kivita katika mzozo wa Syria ambao umeyagharimu maisha ya maelfu ya watu, wengi wao wakiwa raia.

Soma zaidi: Borrell asema utawala wa Bashar al-Assad hauko tayari kwa mabadiliko

Mkuu huyo wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa pia ametaka kufanyike juhudi zaidi za kuwatafuta maelfu ya watu waliopotea, ambao anasema ni pamoja na wale waliofungwa jela zinazoendesha na vikosi vya serikali nchini Syria.

"Kumekuwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na dhulma, matukio ambayo yanaweza kutafsiriwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu," amesema Bachelet.

Maandamano ya kupinga utawala wa kimabavu wa familia ya Rais Bashar al-Assad yalizuka mnamo mwezi Machi mwaka 2011 kusini mwa Syria, japo yalikabiliwa vikali na vikosi vya usalama. Hata hivyo, maandamano hayo yalisambaa haraka katika sehemu nyengine nchini humo.

Zaidi ya watu milioni 11 wameyakimbia makaazi yao

Picha: Bulent Kilic/AFP

Mzozo wa Syria umesababisha zaidi ya watu milioni 11 kuyakimbia makaazi yao.

Vikosi vya usalama vya serikali, vinavyopata uungwaji mkono wa Iran na Urusi vimechukua udhibiti wa maeneo mengi ambayo wakati mmoja yalikuwa chini ya udhibiti wa waasi. Hata hivyo, bado vita vinaendelea katika sehemu kadhaa za Syria.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ametoa mwito wa misaada zaidi ya kibinadamu kupelekwa nchini Syria.

Putin na Erdogan wakutana Moscow kujadili mzozo wa Syria

01:21

This browser does not support the video element.

Guterres amesema hali katika taifa hilo la Mashariki ya Kati ni mbaya mno na kuwa asilimia 60 ya Wasyria wanakabiliwa na kitisho cha ukosefu wa chakula mwaka huu.

"Miaka kumi iliyopita, kukandamiziwa kwa nguvu kwa maandamano ya amani nchini Syria kulifungua njia kwa nchi hiyo kutumbukia kwenye vita. Kwa miaka kumi, dunia imeitazama Syria ikitumbukia kwenye uharibifu mkubwa na umwagaji damu."

Wakati hayo yanaarifiwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani amesema leo kuwa amefanya mazungumzo na mawaziri wenzake wa Urusi na Uturuki mjini Doha juu ya njia za kupeleka misaada ya kibinadamu nchini Syria.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW