1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watu milioni 4.4 duniani hawana uraia wowote

4 Novemba 2023

Umoja wa Mataifa umesema siku ya Jumamosi kuwa watu milioni 4.4 duniani kote hawana uraia wa taifa lolote, ingawa idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na watu hao "kutotiliwa maanani".

Belarus Migration in die EU
Watu wanaoshukiwa kuwa wahamiaji haramu wakiwa mjini Brest, UfaransaPicha: Ales Petrowitsch/DW

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limesema kutokuwa na uraia wa taifa lolote kuna "athari mbaya" huku likitoa wito wa hatua zaidi kuchukuliwa ili kukabiliana na tatizo la kutengwa kwa watu hao.

UNHCR imesema wakiwa hawatambuliwi kama raia wa nchi yoyote, watu wasio na utaifa mara nyingi haki zao hukandamizwa huku wakishindwa pia kupata huduma za msingi. Watu hao mara nyingi hutengwa kisiasa na kiuchumi na hukabiliwa na vitendo vya ubaguzi, uonevu na unyanyasaji wa aina mbalimbali. 

Soma piaMaandamano dhidi ya sheria mpya ya uraia India:       

Taarifa ya shirika hilo imeendelea kuwa takriban watu milioni 4.4 katika jumla ya nchi 95 wanaripotiwa kutokuwa na uraia au kuwa na uraia ambao haujabainishwa rasmi. Ni wazi kwamba takwimu ya kimataifa juu ya watu wasio na utaifa ni kubwa zaidi kuliko iliyotangazwa, na hii ni kutokana na watu hao kutoorodheshwa katika zoezi za kitaifa za kuhesabu watu.    

Watu wakiwa nje ya kambi ya muda huko Kara Tepe- Mavrovouni, Visiwa vya Lesbos Ugiriki:09.09.2020Picha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

UNHCR imeendelea kuwa idadi kubwa ya watu wasio na uraia wowote duniani hutoka kwenye jamii za walio wachache, ambazo tatizo hilo limekuwa likiendelezwa na hivyo kuzidisha vitendo vya ubaguzi na kutengwa ambavyo jamii hizo tayari zinakabiliana navyo.

Mabadiliko ya sera na sheria ni suluhisho

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi la UNHCR Philippo Grandi amesema ingawa  ukosefu wa utaifa  unasababishwa na mambo mengi tofauti, mara nyingi tatizo hilo linaweza kutatuliwa kupitia mabadiliko ya sera na sheria.

Grandi ametoa wito kwa mataifa yote duniani kote kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayeachwa nyuma.Takwimu hizo zimetolewa wakati UNHCR ikiadhimisha mwaka wa tisa wa kampeni yake ya "IBelong" kuhusu suala hilo.    

Soma pia: Wahamiaji wapewa uraia visiwani Zanzibar

Shirika hilo limesisitiza kuwa mnamo mwaka 2023, Kenya, Kyrgyzstan, Moldova, Macedonia Kaskazini, Ureno na Tanzania zilipiga hatua muhimu katika suala hilo la watu wasiokuwa na utaifa, huku Jamhuri ya Kongo ikiwa nchi ya hivi punde zaidi kukubaliana na Mikataba ya kurekebisha suala la kutokuwa na utaifa.

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi la UNHCR Philippo Grandi akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswisi, 12.06.2023Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Kwa ujumla, nchi 97 sasa zilisaini Mkataba wa mwaka 1954 unaohusiana na Hadhi ya Watu Wasio na Uraia, huku nchi 79 zikiwa sehemu ya Mkataba wa mwaka 1961 wa kupunguza idadi ya watu wasio na utaifa.  

Soma pia: Wanaoomba hifadhi kupata haki ya kuishi moja kwa moja nchini Ujerumani.

Grandi amesema mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na tatizo hilo ni chanya na ameyapongeza mataifa kwa kuchukua hatua stahiki. Lakini amesema haitoshi kutokana na kuongezeka kwa uhamaji duniani hasa wa watu wanaolazimika kuyahama makazi ya.

Kamishna huyo mkuu wa UNHCR amehitimisha kwa kusema kuwa mamilioni ya watu wanatengwa na kunyimwa haki zao za msingi kama binadamu, ikiwa ni pamoja na kushiriki na kuchangia katika ustawi wa jamii. Grandi amesisitiza kuwa vitendo vya kutengwa kwa watu wasiokuwa na utaifa si haki na ni lazima vishughulikiwe.

(Chanzo:AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW