UN: Uhalifu dhidi ya ubinaadamu wafanyika Burundi
4 Septemba 2017Katika ripoti ya tume hiyo iliyochapishwa leo kuhusu Burundi imeelezwa kwamba mauaji, utesaji, vitendo vya ubakaji, manyanyaso, kutoweka kwa watu pamoja na watu kukamatwa ovyo ni mambo ambayo yamekuwa yakifanyika tangu Aprili, 2015 na yanaendelea kushuhudiwa hadi wakati huu.
Ripoti hiyo inasema kwamba maafisa wa ngazi ya juu kutoka vyombo vya usalama wa taifa wa Burundi pamoja na polisi, maafisa wa kijeshi na wanachama wa tawi la vijana la chama tawala linalojulikana kama Imbonerakure ni miongoni mwa watuhumiwa wa vitendo hivyo.
Tume hiyo imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kufungua kesi haraka iwezekanavyo kwa sababu kuna mazingira yanayomaanisha kuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu umefanyika na unaendelea kutekelezwa nchini Burundi.
Zaidi ya mashahidi 500 walihojiwa katika kipindi cha miezi kadhaa ya uchunguzi ikiwemo Warundi wengi wanaoishi nje kama wakimbizi na wengine walioko bado nchini Burundi ambao muda wote wanahatarisha maisha yao.
Ripoti pia inasema kwamba matukio yote ya wahanga familia zao na mashahidi yamepitiwa kwa umakini na kuthibitishwa.