1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Uhalifu wa kivita unafanyika Yemen

Caro Robi
28 Agosti 2018

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema pande zinazozana Yemen huenda zimehusika katika uhalifu wa kivita, wakitaja mashambulizi makali ya anga, udhalilishaji wa kingono na watoto kutumikishwa kama wapiganaji.

Yemen - al-Hudaida - Soldat
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Gambrell

Katika ripoti yao ya kwanza, kundi la wachunguzi wa Umoja wa Mataifa limesema kuna ushahidi wa kutosha kudhihirisha kuwa wanaohusika katika mzozo wa Yemen, wamekiuka sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu.

Mzozo huo wa Yemen, ambayo ni mojawapo ya nchi masikini zaidi duniani, umesababisha kile Umoja wa Mataifa ulichokiita mojawapo ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Ukiukaji wa haki unafanywa na pande zote

Kundi hilo la wataalamu huru wa kimataifa na wa kanda ya Mashariki ya Kati lililoundwa na Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu mwezi Septemba mwaka jana, limeelezea vitendo kadhaa vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa na pande zote mbili zinazozana Yemen.

Mtoto anayetumikishwa Jeshini akiwa amebeba bundukiPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Mohammed

Taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kundi hilo Kamel Jendoubi imesema kuna ushahidi mdogo wa kuonesha juhudi zozote za pande husika kupunguza athari za mzozo dhidi ya raia.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imegundua kuwa mashambulizi ya angani yanayofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ndiyo yamesababisha maafa makubwa dhidi ya raia kwani yanalenga makazi, masoko, mazishi, harusi, vituo vya kuwazuia watu, boti za kubeba raia na vituo vya afya. Robo tatu ya idadi ya Wayemen milioni 20 wanategemea misaada ya kibinadamu.

Raia ndiyo waathiriwa wakubwa

Mapema leo, Misururu ya mashambulizi makali ya angani yameripotiwa kulenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Yemen ulioko katika mji mkuu Sanaa, unaodhibitiwa na waasi na kambi ya jeshi la angani iliyoko mkabala na uwanja huo wa ndege. Waasi wa Houthi wanawaulumu wanajeshi wa serikali kwa mashambulizi hayo.

Mwanamke akiwa hospitalini akisubiri matibabuPicha: Reuters/K. Abdullah

Mashambulizi hayo yaliyoulenga uwanja huo wa ndege ambao hautumiki sana isipokuwa na ndege za Umoja wa Mataifa na kambi ya kijeshi ya Al Dailami yanakuja saa chache baada ya Wahouthi kusema wameulenga uwanja wa ndege wa Dubai kwa shambulizi la ndege isioendeshwa na rubani, madai ambayo yamekanusha Umoja wa Falme za Kiarabu. Saudi Arabia imesema imenasa kombora lililorushwa na waasi wa Houthi katika jimbo la Najran.

Hayo yanaripotiwa wakati ambapo Umoja wa Mataifa unapanga mkutano wa kutafuta amani kati ya serikali ya Yemen na waasi wa Houthi utakaofanyika tarehe 6 mwezi ujao mjini Geneva.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaangazia ukiukwaji wa haki za binadamu kuanzia mwezi Septemba mwaka 2014 hadi mwezi Juni mwaka huu, hivyo haiangazii mlolongo wa mashambulizi ya siku za hivi karibuni ambayo yamewaua watoto kadhaa wanaoishi katika maeneoo yanayodhibitiwa na waasi. Mashambulizi hayo yamelaaniwa vikali na Jumuiya ya Kimatiafa.

Muungano huo wa kijeshi haujakanusha au kuthibitisha kufanya mashambulizi mawili ya anga Alhamisi iliyopita ambayo Umoja wa Mataifa umesema yamewaua takriban watoto 26 na wanawake wanne kusini mwa mji wa Hodeida.

Vita vya Yemen vimesababisha vifo vya takriban 10,000 tangu mwezi machi mwaka 2015, wakati muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulipojingiiza katika mzozo kati ya waasi wa Houthi na serikali ya Rais Abedrabbo Mansour Hadi.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri:mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW