1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Ujerumani ni chachu ya amani Duniani

18 Desemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameipongeza Ujerumani kwa kuwa chachu ya amani na nguzo ya ushirikiano wa kimataifa. Antonio Guterres ameyazungumza hayo katika hotuba aliyoitowa mbele ya bunge la Ujerumani Ijumaa.

Berlin | UN-Generalsekretär Guterres im Bundestag
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Hotuba ya Guterres katika bunge la Ujerumani, Bundestag, ambayo ni ya maadhimisho ya 75 tangu kuundwa Umoja wa Mataifa, imegusia masuala mbali mbali kuanzia virusi vya Corona hadi mabadiliko ya tabia nchi. Guterres amesema akiwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anashuhudia kila siku kwa jinsi gani Ujerumani yenye historia ya umakini na uwabijikaji inavyobeba dhima ya uongozi duniani.

Guterres ametowa hotuba hiyo kwa lugha ya Kijerumani kwa kujiamini kabisa. Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameitaja Ujerumani kuwa ni nchi mshirika muhimu kabisa duniani katika kutafuta amani akitowa mifano ya ujumbe wa nchi hiyo nchini Afghanistan pamoja na eneo la Sahel barani Afrika ambako jeshi la Ujerumani linasaidia kulinda amani.

Chanjo zinastahili kuwa bidhaa ya umma

Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu amelizungumzia janga la virusi vya Corona akisema ni changamoto ya kidunia na kwa hivyo chanjo ya kupambana na virusi hivyo inahitaji kutazamwa kama bidhaa ya ulimwengu kwa ujumla wake.

Guterres akiwa katika bunge la Ujerumani, BundestagPicha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

"Sasa ni muhimu kuhakikisha kwamba chanjo zinashughulikiwa kama bidhaa ya uma ambayo inapaswa kumfikia kila mmoja na kila mahala kwa gharama nafuu," alisema Guterres.

Guterres pia ametowa shukurani zake za dhati kwa mchango uliotolewa na raia wa Kijerumani Ugur Sahin na Ozlem Tureci, waasisisi wa kampuni ya BioNTech ambayo chanjo yake iliyoitengeneza kwa ushirikiano na kampuni kubwa ya madawa ya Marekani imeidhinishwa  katika nchi kadhaa. Amesema Umoja wa Mataifa unashughulikia suala la kujenga imani juu ya chanjo kwa kuzingatia sayansi na hali halisi.

Vita vya silaha si kitisho kikubwa, ila vita vya mazingira

Ama kwa upande mwingine, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amezungumzia suala la mabadiliko ya tabia nchi akisema msukumo unaoshuhudiwa katika suala la Brexit barani Ulaya  ndio unaotakiwa pia katika kufikiwa sera ya pamoja kuhusu mambo ya nje na usalama. Amesema msukumo huo ungekuwepo pia kwa mfano katika suala la wakimbizi au katika utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kuhusu mazingira.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: German Chancellery/Pool/AA/picture alliance

"Kitisho kikubwa katika usalama wetu hakitokani na vita vya silaha, bali vita vya kujitowa muhanga dhidi ya mazingira. Kitisho cha mazingira ni cha uhakika," aliongeza Guterres.

Baada ya hotuba yake hiyo katika bunge la Ujerumani, Guterres amepangiwa pia kuzungumza na Kansela Angela Merkel na Rais Frank-Walter Steinmeier.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW