UN: Ukatili dhidi ya watoto waongezeka pakubwa 2020
22 Juni 2021Idadi ya watoto waliotekwa nyara na kubakwa katika maeneo yenye mizozo iliongezeka mnamo mwaka 2020, kulingana na ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu.
Ripoti ya kila mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa baraza la usalama la umoja huo juu ya watoto na mizozo, iliangazia madhila wanayopitia watoto ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, utekaji nyara wa watoto, utumikishwaji wa watoto katika jeshi pamoja na mashambulizi yanayolenga shule na hospitali.
Soma zaidi: Ajira kwa watoto yaongezeka ulimwenguni
Mwakilishi maalum wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia watoto Virginia Gamba amesema,
"Watoto wa Israel na Palestina hawastahili kufanyiwa hivi. Kwa kweli hawastihili. Nadhani kuna wakati itabidi kufanyike mazungumzo ya kuwalinda watoto. Na lazima hilo lifanyike kwa sababu sidhani watoto wa Israel na Palestina wanalala vizuri usiku. Tunapaswa kulinda watoto, Hakuna namna nyengine. Lazima kuwepo na suluhisho la amani juu ya suala hili.
Ripoti hiyo iliainisha visa vya unyanyasaji dhidi ya watoto 19,379 katika maeneo 21 yenye mizozo.
Vile vile, ripoti hiyo imeongeza kuwa jumla ya watoto 8,521 walitumika kama wanajeshi katika maeneo mbalimbali ya mizozo mwaka uliopita wakati watoto 2, 674 waliuawa na wengine 5, 748 walijeruhiwa.
Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afghanistan, Syria na Yemen ndio nchi zilizoandikisha idadi kubwa ya visa vya unyanyasaji dhidi watoto kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2020.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa pia imejumuisha orodha ya watu wanaohusika ikilenga kuwaweka wazi ili kuwashinikiza kuweka mikakati ya kulinda haki za watoto.
Hata hivyo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeukosoa Umoja wa Mataifa kwa kutoijumuisha Israel na Saudia Arabia kwenye orodha ya mataifa ambamo haki za watoto zinakiukwa.
Wakati Israel haijawahi kuwepo kwenye orodha hiyo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliondolewa kwenye orodha hiyo mnamo mwaka 2020, miaka kadhaa baada ya kutajwa na kukosolewa kwa madai ya kuua na kuwajeruhi watoto nchini Yemen.
Wanadiplomasia wamewahi kusema kuwa Saudi Arabia na Israel zilitumia ushawishi wao na kuweka shinikizo wasijumuishe kwenye orodha hiyo.
Aidha jeshi la Myanmar na vikosi vya usalama vya serikali ya Syria pia vimetajwa kwenye orodha hiyo kwa kukiuka haki za watoto.