1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Urusi inawachukua kwa nguvu watoto wa Ukraine

8 Septemba 2022

Umoja wa Mataifa na Marekani wametaja kile walichokiita tuhuma za kuaminika kwamba vikosi vya Moscow vinawapeleka kwa nguvu watoto wa Ukraine nchini Urusi. Urusi inapinga ikisema raia hao walisajiliwa kwa hiari

Ukraine, Lviv | Settlement for displaced people in Lviv
Picha: Mykola Tys/picture alliance

Akizungumza mjini New York katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa na Marekani na Albania, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binaadamu Ilze Brands Kehris amesema vikosi vya Urusi vinawaweka Waukraine katika maeneo yaliyokamatwa kupitia vituo vya ukaguzi wa usalama ambavyo vimehusishwa na matukio mengi ya ukiukaji wa haki za binaadamu. "Tuna wasiwasi maafisa wa Urusi wanautumia utaratibu uliorahisishwa wa kuwapa uraia wa Urusi watoto wasio chini ya ulezi wa wazazi, na kuwa watoto hawa wataweza kuasiliwa na familia za Kirusi."

Soma zaidi: UN: Zaidi ya raia milioni 4.9 wa Ukraine wameikimbia nchi hiyo

Balozi wa Marekani Linda Thomas-GreenfieldPicha: Yuki Iwamura/AP/picture alliance

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alisema makadirio kutoka kwa duru mbalimbali, ikiwemo serikali ya Urusi, zinaonyesha maafisa wa Urusi wamewahoji, kuwakamata na kuwahamisha kwa nguvu kati ya Waukraine 900,000 na milioni 1.6. 

Soma pia: Idadi ya waliokimbia Ukraine yavuka watu milioni 6

Amesema makadirio hayo yanaonyesha kuwa maelfu ya Watoto wamepenyezwa, baadhi wakitenganishwa na familia zao na kuchukuliwa kutoka vituo vya yatima kabla ya kupewa kwa familia za Kirusi. Kwa mujibu wa taarifa ya Marekani, zaidi ya Watoto 1,800 walihamishwa kutoka maeneo ya Ukraine yanayodhibitiwa na Urusi na kupelekwa Urusi mwezi Julai pekee.

Soma pia: Athari za vita kwa watoto wanaolindwa na serikali Ukraine

Mjini Washington, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imesema ofisi ya Rais wa Urusi Vladmir Putin inasimamia moja kwa moja uhamishaji wa Waukraine kwenda Urusi, na inafanya hivyo kama sehemu ya mpango wa kuyakwapua maeneo iliyoyakamata.

Urusi ilipuuza mara moja madai hayo ikisema ni ndoto za kubuni ikisema ni uvumbuzi wa karibuni wa kampeni ya upotoshaji wa Magharibi.

Balozi wa Urusi Vassily NabenziaPicha: Yuki Iwamura/AP/picture alliance

Lakini Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vasily Nebenzia ameyaita madai hayo kuwa yasiyo na msingi, akisema kinachofanyika ni kusajiliwa kwa hiari nchini Urusi kwa Waukraine wanaokimbia vita. "Kama tunazungmzia kutambua, miongoni mwa watu hao wale wanaotaka kuja Urusi, raia wa Ukraine ambao walikuwa wapigania taifa au wanajeshi wa Ukraine walioshiriki katika uhalifu dhidi ya raia, basi huo ni utaratibu wa kawaida kwa jeshi lolote ulimwenguni."

Amesema zaidi ya Waukraine milioni 3.7, wakiwemo Watoto 600,000 wamekwenda Urusi au maeneo ya kujitenga yanayodhibitiwa na Urusi mashariki mwa Ukraine, lakini hawako magerezani.

Nebenzia amesema Waukraine hao walipitia usajili na sio utaratibu wa kupenyeza, sawa tu na wakimbizi wa Ukraine nchini Poland na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya

Jana usiku, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema wanajeshi wa Kyiv wameyakomboa maeneo kadhaa katika mkoa wa Kharkiv, ijapokuwa alikataa kuyataja. Taasisi ya Marekani ya Utafiti wa Vita, ambayo inafuatilia kwa kina mapigano hayo, imesema shambulizi la Ukraine lilikuwa karibu na Balakliya na huenda liliwarudisha wanajeshi wa Urusi nyuma katika upande wa kaskauini wa mito ya Severskyi Donets na Serednya Balakliika.

AFP/AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW