1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Urusi yafanya uhalifu dhidi ya ubinadamu

28 Oktoba 2025

Urusi imefanya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kuwalazimisha watu kukimbia eneo linaloshikiliwa na Ukraine kupitia mashambulizi ya mara kwa mara ya droni. Haya ni kulingana na ripoti ya tume ya UN.

Ukraine Mei 21, 2025 | Mji wa Pokrovsk
Wanajeshi wa Ukraine watafuta wakazi wa Pokrovsk kuwahamisha kutoka eneo hilo kutokana na mashambulizi ya UrusiPicha: Anatolii Stepanov/REUTERS

Ripoti ya tume hiyo iliyoundwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa muda mfupi baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo mwaka 2022, imesema mamlaka ya Urusi iliratibu kimkakati hatua za kuwafukuza raia wa Ukraine kutoka kwenye makazi yao kwa matumizi ya droni hizo pamoja na uhamishaji wa nguvu.

Urusi yadaiwa kufanya uhalifu wa kivita

Pia imesema Urusi ilifanya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa mauaji katika maeneo makubwa zaidi ya eneo hilo la mashariki kuliko ilivyothibitishwa awali.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa Urusi ilifanya uhalifu wa kivita kwa kuelekeza kwa makusudi mashambulizi dhidi ya raia na mali ya kiraia, pamoja na unyanyasaji wa kibinadamu na ukiukaji wa haki za binadamu.

Imeendelea kusema tume hiyo imebainisha kuwa mashambulizi hayo yamewalazimu maelfu ya watu kukimbia.

Ukraine yaimarisha tahadhari katika mji wa Pokrovsk

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema kuwa takriban raia 200 wa Urusi wanaishi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Pokrovsk.

Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Julien Mattia/Le Pictorium/MAXPPP/picture alliance

Katika matamshi yaliochapishwa leo na vyombo vya habari, Zelensky amesema hilo imedhihirika kupitia droni na kwamba kwa sasa mji huo ndio shabaha kuu ya Urusi.

Zelensky ameongeza kusema kuwa amezungumza na jeshi la Ukraine na tahadhari maalum inalenga Pokrovsk na maeneo ya jirani.

Amesisitiza kuwa hapo ndipo wavamizi walipoongeza vikosi vyao na kwenye kiwango kikubwa cha mashambulizi.

Ukraine yasema inahitaji msaada zaidi wa Ulaya

Rais Zelensky amesema kuwa Ukraine inahitaji msaada wa kifedha wa Ulaya ili kuendelea kupambana na wanajeshi wa Urusi kwa miaka mingine miwili au mitatu.

Katika matamshi yake yaliyochapishwa leo, Zelensky amesema alisisitiza haya kwa mara nyingine tena kwa viongozi wa Ulaya na akawaambia hawataendelea kupigana tena kwa miongo, lakini kwa muda lazima waonyeshe kuwa wataweza kutoa msaada wa kifedha kwa Ukraine.  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW